POLISI WATIWA MBARONI KWA KUKUTWA NA MENO YA TEMBO.
Na Antony Sollo .
6/1/2013
JESHI la polisi mkoani Mara linawashikilia askari polisi wawili kutoka mkoani Kagera pamoja na raia wawili baada ya kukutwa na vipande 17 vya meno ya tembo.
Akiongea na Jamboleo kamanda wa polisi mkoani Mara Absalom Mwakyoma alisema kuwa watu hao walikamatwa usiku wa kuamkia January 6 mwaka huu majira ya saa 8 usiku huko katika kijiji cha Lwamchanga tarafa ya Logoro wilayani Serengeti mkoani Mara.
Mwakyoma ameeleza kuwa siku hiyo ya tukio askari polisi waliokuwa doria kwa kushirikiana na askari wa kikosi cha wanyama pori waliwakamata watu wawili,Boniface Kurwa 31 mkazi wa Geita akiwa na pikipiki yenye namba za usajili T874 CCC aina ya Sunlg ambayo mmiliki wake bado hajafamika na mwenzake aliyefahamika kwa jina moja la Nyarata mkazi wa mjini Mugumu ambaye pia alikuwa na pikipiki namba T834 ZPH ainaya Toyo ambayo nayo mmiliki wake bado hajafahamika.
Kwa mujibu wa kamanda Mwakyoma wananchi hao baada ya kusimamishwa na askari hao walitupa pikipiki na kukimbia lakini Polisi walifanikiwa kumkamata Boniface Kurwa ambapo mwenzake alifanikiwa kukimbia na polisi walipokagua pikipiki hizo walikuta zimepakia vipande 17 vya meno ya tembo ambapo inasemekana kuwa idadi ya men ohayo inaonyesha kuwa ni sawa na tembo watatu waliouwawa.
Akifafanua zaidi Kamanda huyo alisema kuwa baada ya kukamatwa ,mtuhumiwa Kurwa alitoa ushirikiano mkubwa kwa jeshi la Polisi ambapo aliwaambia Askari waliokuwa wakimhoji kuwa waliowatuma pembe hizo wapo katika hoteli moja iitwayo Gaalax ya mjini Mugumu ambapo Polisi walikwenda na kuwakuta askari wawili mmoja mwenye namba E9172 D/C,Coplo David ambaye ni wa kituo cha polisi Biharamulo na F 5553 D/C Jerad wa kitengo cha upelelezi wa makosa ya jinai Bukoba.
‘’Baada ya kuhojiwa askari hao walikiri na wakadai kuwa wamefika huku baada ya kuelekezwa na mtu mmoja aitwaye Boniface Emanuel maarufu kama Mnyarwanda ambaye ni mkazi wa huko Biharamulo’’alisema kamanda Mwakyoma.
Aliongeza kuwa askari hao walikuwa na gari dogo lenye namba za usajili namba T403 BTK aina ya Carina mali ya D/C Gerad ambalo pia linashikiliwa na polisi,na kwamba watuhumiwa wote wanatarajia kufikishwa mahakamani muda wote upelelezi wa awali utakapokamilika.
Hata hivyo kamanda huyo ametoa wito kwa watumishi wa serikali kutambua kuwa hawako juu ya sheri na kwamba waache kujihusisha na vitendo vya kuhujumu uchumi kwani wakikamatwa sheria itachukuwa mkondo wake.