Monday, January 14, 2013

WATANO WAPIGWA RISASI MGODI WA MWADUI


WATANO WAPIGWA RISASI MGODI WA MWADUI
Na Antony Sollo  - Kishapu.
WATU watano wakazi wa Kata ya Mwadui Luhumbo, wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga wamepigwa risasi baada ya kuingia mgodini kwa lengo la kuchukua mabaki ya mchanga wa almasi.

Mashuhuda wa tukio hilo waliliambia Tanzania Daima Jumapili kuwa, tukio hilo lilitokea Januari 7, mwaka huu majira ya saa 2:00 usiku ambapo watu hao waliingia mgodini kwa ajili ya kuchukua mabaki ya mchanga wa madini ya almasi ili wakasafishe na kuuza.

Walieleza kuwa watu hao wakiwa katika harakati za kuchukua mabaki ya mchanga ndipo walinzi wa mgodi huo walipowafyatulia risasi zilizowajeruhi mguuni.

Waliwataja majeruhi wawili waliokutwa na mkasa huo ni George Busiga (31) na Hamidu Hamidu (28) ambao wamelazwa katika Hospitali ya Mwadui na majeruhi wengine hawajafahamika majina yao.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala, alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo, alisema kuwa hana taarifa na kuahidi kulifuatilia

Sunday, January 6, 2013

POLISI WATIWA MBARONI KWA KUKUTWA NA MENO YA TEMBO.


POLISI  WATIWA MBARONI KWA KUKUTWA NA MENO YA TEMBO.

Na  Antony Sollo .

6/1/2013

JESHI la polisi mkoani Mara linawashikilia askari polisi wawili kutoka mkoani Kagera pamoja na  raia wawili  baada ya kukutwa na vipande 17 vya meno ya tembo.

Akiongea na Jamboleo kamanda wa polisi mkoani Mara Absalom Mwakyoma alisema  kuwa watu hao walikamatwa usiku wa kuamkia January 6 mwaka huu majira ya saa 8 usiku huko katika kijiji cha Lwamchanga tarafa ya Logoro wilayani Serengeti mkoani Mara.

Mwakyoma ameeleza kuwa siku hiyo ya tukio askari polisi waliokuwa doria kwa kushirikiana na askari wa kikosi cha wanyama pori waliwakamata watu wawili,Boniface Kurwa 31 mkazi wa Geita akiwa na pikipiki yenye namba za usajili T874 CCC aina ya Sunlg ambayo mmiliki wake bado hajafamika  na mwenzake aliyefahamika kwa jina moja la Nyarata mkazi wa mjini Mugumu ambaye pia alikuwa na pikipiki namba T834 ZPH ainaya Toyo ambayo nayo mmiliki wake bado hajafahamika.

Kwa mujibu  wa kamanda Mwakyoma  wananchi hao baada ya kusimamishwa na askari hao walitupa pikipiki na kukimbia lakini Polisi walifanikiwa kumkamata  Boniface Kurwa  ambapo mwenzake alifanikiwa  kukimbia na polisi walipokagua pikipiki hizo walikuta zimepakia vipande 17 vya meno ya tembo ambapo inasemekana kuwa idadi ya men ohayo inaonyesha kuwa ni sawa na tembo watatu waliouwawa.

Akifafanua  zaidi  Kamanda huyo alisema kuwa baada ya kukamatwa ,mtuhumiwa Kurwa alitoa ushirikiano mkubwa kwa  jeshi la Polisi ambapo aliwaambia Askari waliokuwa wakimhoji kuwa waliowatuma pembe hizo wapo katika hoteli moja iitwayo Gaalax ya mjini Mugumu ambapo Polisi walikwenda na kuwakuta askari wawili mmoja mwenye namba E9172 D/C,Coplo David ambaye ni wa kituo cha polisi Biharamulo na F 5553 D/C Jerad wa kitengo cha upelelezi wa makosa ya jinai Bukoba.

‘’Baada ya kuhojiwa askari hao walikiri na wakadai kuwa wamefika huku baada ya kuelekezwa na mtu mmoja aitwaye Boniface Emanuel maarufu kama Mnyarwanda ambaye ni mkazi wa huko Biharamulo’’alisema kamanda Mwakyoma.

Aliongeza kuwa askari hao walikuwa na gari dogo lenye namba za usajili namba T403 BTK aina ya Carina mali ya D/C Gerad  ambalo pia linashikiliwa na polisi,na kwamba watuhumiwa wote wanatarajia kufikishwa mahakamani muda wote upelelezi wa awali utakapokamilika.

Hata hivyo kamanda huyo ametoa wito kwa watumishi wa serikali kutambua kuwa hawako juu ya sheri na kwamba waache kujihusisha na vitendo vya kuhujumu uchumi kwani wakikamatwa  sheria itachukuwa mkondo wake.