Na Antony Sollo Geita
Wachungaji
wa Makanisa ya Grory of God, PVTC , CGT yaliyoko Mtaa wa Moringe Kata ya
Buhalahala Mkoani Geita wameingia katika mvutano mkali na Uongozi wa Serikali
ya Mtaa huo wakidaiwa kuvamia maeneo ya Shule ya awali ya Moringe Tanzania Daima
linaweza kuripoti.
Licha ya Viongozi
wa Makanisa hayo kuamuriwa kuondoka katika maeneo hayo na Mratibu wa baraza la
Mazingira NEMC kutoka Halmashauri ya Mji wa Geita,Utekelezaji wa amri hiyo
umekuwa ni mgumu kutokana na wachungaji hao kukaidi amri hiyo ambapo kanisa
lililokuwa limeezekwa kwa maturubai sasa limeezekwa kwa kasi kwa kutumia bati.
Akizunguma
na Tanzania Daima Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Moringe Adriano Rwechungura
alisema kuwa,Viongozi hao wamekuwa wakiombwa mara kadhaa kuhama na kutafuta
maeneo yanayofaa kwa kuendesha ibada zao lakini wameshindwa kuheshimu taratibu
za Serikali na kuendeleza malumbano makubwa ambapo hadi sasa kuna mvutano
mkubwa kati ya Serikali na taasisi hizo.
“Tumekuwa
tukiwasihi viongozi hao wa Makanisa wafuate taratibu zilizowekwa na Serikali
lakini hawataki na ni kwamba uwepo wa Makanisa katika eneo la Shule hiyo ni uvunjaji
wa Sheria na ukwamishaji wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu kwani kumekuwa na
kelele nyingi zinazotokana na ibada zinazofanywa na waumini hao”alisema
Rwechungura.
Kwa upande
wake Msimamizi wa Shule ya awali ya Moringe Mwalimu Msafiri Masolwa alikiri kuwepo
kwa kero katika eneo la Shule hiyo na kusema
kuwa Serikali itafakari juu ya mwingiliano wa taasisi hizo iwapo Shule au
kanisa ibaki katika eneo hilo kufuatana na uhitaji wa wananchi wenyewe .
‘Taratibu
ziangaliwe kwamba ni taasisi ipi ilikuwa ya kwanza kuanzisha shughuli zake
katika eneo hilo na iwapo shule itaonekana ilikuwa ya kwanza ibaki na kama
Kanisa lilikuwa la kwanza kuwepo katika eneo hilo basi hakuna budi kubakia
katika eneo hilo alisema Masolwa”
Akizungumza
na gazeti hili Katibu wa Tawi la Moringe kupitia Chama cha Mapiduzi Robert
Maganga alisema kuwa katika kulifuatilia
suala wamekutana na mratibu wa baraza la Mazingira Mkoa wa Geita na kuambiwa
kuwa,viongozi hao waliamuriwa kuondoka katika maeneo ya shule hiyo ndani ya siku
saba lakini utekelezaji hujafanyika hadi sasa.
Kwa
Mujibu wa Rwechungura Wengine walioingia
mgogoro na Serikali ya Mtaa wa Moringe ni pamoja na familia nne ambazo ziko
katika eneo la Shule hiyo na kwamba zilishapewa notsi ya kupisha eneo la Shule
na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita lakini wanafamilia hao walikataa
kufanyiwa tathimini na kwamba Ofisi ya Mwenyekiti wa Mtaa inasubiri Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Mji wa Geita atoe notsi kwa mara ya pili.
Kuhusu
ujenzi wa barabara za Mtaa, Mwenyekiti wa Mtaa wa Moringe Adriano Rwechungura alimtuhumu
Diwani wa Kata ya Buhalahala Elias Kabese kwa kuhujumu miradi mbalimbali ya
maendeleo katika Mtaa wake.
“Diwani
wetu hajatutendea haki kwani amehujumu miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa
barabara kwamba March 2017 zilitolewa fedha za mfuko wa jimbo na Mbunge wetu Mheshimiwa Costantine Kanyasu kiasi cha shilingi mil 4 ambazo zilipangwa kwa
ajili kuchongewa barabara kila Mtaa kwa masaa 8 lakini Diwani kwa sababu
anazozijua yeye ameutenga Mtaa wetu na hadi sasa hakuna barabara hata moja
iliyochongwa kupitia fedha za mfuko wa Jimbo zilizotolewa na Mbunge wetu na
kwamba kufuatia hali hiyo ya kibaguzi iliyoonyeshwa na Diwani huyo wananchi wakazi
wa Mtaa wa Moringe wameamua kuchangishana wenyewe na kwamba Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita
imekubali kutoa Greda kwa ajili ya
kuchonga barabara za Mtaa”.alisema Rwechungura.
Mbunge wa
Jimbo la Geita Mjini Costantine Kanyasu alipotafutwa na Mwandishi wa gazeti
hili ili kuzungumzia fedha za mfuko wa Jimbo alizotoa na tuhuma za ubaguzi unaofanywa
na Diwani wa Kata ya Buhalahala Kanyasu likiri kutoa fedha hizo kwa ajili ya
matengenezo ya barabara za Mtaa, lakini Mbunge huyo alionyesha wasiwasi wake kuhusu
uadilifu wa Diwani huyo.
“ Usishangae
ukisikia fedha hizo hazijafanya kazi iliyokusudiwa maana huyo bwana mdogo ni
mjanjamjanja sana,sina uhakika kuhusu matumizi ya fedha hizo lakini kufuatia
malalamiko hayo tutafanya utaratibu katika vikao vyetu vya halmashauri na ikibidi
tutamtuma Mkaguzi wa ndani ili kwenda kujiridhisha juu ya matumizi ya fedha
hizo na ikibainika kuwa kulikuwa na matumizi tofauti na malengo ya kutolewa kwa
fedha hizo hatua stahiki zitachukuliwa”alisema Kanyasu.
Kanyasu
ameliambia Tanzania Daima kuwa katika awamu ya pili atatoa kipaumbele kwa
wakazi wa Mtaa wa Moringe kuwachongea barabara nzuri ili kuharakisha maendeleo
yao.
MWISHO