WATANO WAPIGWA RISASI MGODI WA MWADUI
Na Antony Sollo - Kishapu.
WATU watano wakazi wa Kata ya Mwadui Luhumbo, wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga wamepigwa risasi baada ya kuingia mgodini kwa lengo la kuchukua mabaki ya mchanga wa almasi.Mashuhuda wa tukio hilo waliliambia Tanzania Daima Jumapili kuwa, tukio hilo lilitokea Januari 7, mwaka huu majira ya saa 2:00 usiku ambapo watu hao waliingia mgodini kwa ajili ya kuchukua mabaki ya mchanga wa madini ya almasi ili wakasafishe na kuuza.
Walieleza kuwa watu hao wakiwa katika harakati za kuchukua mabaki ya mchanga ndipo walinzi wa mgodi huo walipowafyatulia risasi zilizowajeruhi mguuni.
Waliwataja majeruhi wawili waliokutwa na mkasa huo ni George Busiga (31) na Hamidu Hamidu (28) ambao wamelazwa katika Hospitali ya Mwadui na majeruhi wengine hawajafahamika majina yao.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala, alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo, alisema kuwa hana taarifa na kuahidi kulifuatilia