Monday, February 19, 2018

Hongera Waziri Mkuu kufanya ziara Mwanza

Antony Sollo  Misungwi

Ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Jijini Mwanza imekuwa ya mafanikio,hii ni baada ya kubaini mambo uozo lakini haya ni kwa uchache kutokana na siri kubwa iliyofichika kutokana uozo mwingi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza.

Historia ya kuwepo kwa Uozo Misungwi.

Wilaya ya Misungwi ni moja kati ya Wilaya kongwe nchini ambazo zimekuwa zikiongoza kwa kupata hati chafu na imekuwa bahati kwa Mawaziri Wakuu wa awamu ya Nne na ya tano ambao wote wamebahatika kukumbana na uozo jambo lililopelekea kuwatumbua watumishi wachache wa Halmashauri hiyo huku vinara wakiachwa kutokana na kuwepo kwa mnyororo mkubwa ambao umetengenezwa maalumu kwa ajili ya upigaji dili.

Katika ziara yake hivi karibuni,Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Khassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi,  Alphonce Sebukoto,  na kuagiza achungunzwe na vyombo husika.

Waziri Mkuu alifikia hatua hiyo baada Mwanasheria huyo kuonekana kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kushindwa kuishauri vyema halmashauri hiyo na kuisababishia hasara ya sh. milioni 279.


Majaliwa alimsimamisha kazi Sebukoto 19februari mwaka huu wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa halmashauri hiyo akiwa katika ziara ya siku tano ya kikazi mkoani Mwanza ambapo waziri Mkuu alisema.

“Mwanasheria utasimama kazi kuanzia leo na tuhuma zako zitachunguzwa kikamilifu na vyombo husika na uchunguzi ukibaini kama huna kosa utarudi kazini. hatutakuonea lakini hatuwezi kukuvumilia kwa utaratibu huo ulioufanya,” alisema Majaliwa.

Imeelezwa kuwa Novemba 2017 wakati alipokuwa anakaimu nafasi ya Ukurugenzi Mwanasheria huyo aliidhinisha malipo ya sh. milioni 279 zilipwe katika akaunti binafsi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Antony Bahebe.

Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri Mkuu Bahebe aliishtaki halmashauri hiyo akidai kulipwa fedha kwa ajili ya kazi ya ukandarasi wa mradi wa maji Igenge uliojengwa na kampuni ya ukandarasi ya Seekevim ambapo alisema  mradi huo ulianza 2014 na ulitakiwa ukamilike 2015,ambapo  Mwanasheria huyo aliidhinisha malipo hayo wakati ambao tayari hati maalumu ya uwakilishi ilikuwa imekwisha tangu Desemba 2015.

“Mwanasheria amemlipa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kufanya kazi na Halmashauri baada ya kuifikisha Halmashauri yake Mahakamani. Amemlipa fedha wakati kazi yenyewe ilikuwa haijaisha na aliharakisha malipo hayo kipindi ambacho Mkurugenzi hayupo, ”alisema Majaliwa huku  akiwakumbusha watumishi wa umma kuzingatia maadili ya utumishi na matakwa ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akifafanua Majaliwa alisema fedha alizolipwa Bahebe zingeweza kutumika katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri hiyo.

Katika ziara hiyo Waziri Mkuu alifungua mabweni ya watoto wenye mahitaji maalumu katika shule ya msingi ya Mitindo iliyoko wilayani Misungwi na pamoja na kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Ukiacha na kipande hicho cha uozo uliofichwa,Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi imekuwa na historia mbaya kwa watendaji wa Wilaya hiyo kutafuna fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo wamekuwa wakibuni mbinu mbalimbali kuwahadaa wananchi.

Mwaka 2016 Kaimu Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Sanjo Charles Bulugu,alimchongea kwa Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Eliud Mwaiteleke kwa kutoa taarifa za uongo katika mkutano wa Serikali ya Kijiji cha Sanjo akisema  kuwa,Mkurugenzi huyo alishindwa kufika katika mkutano wa kijijinihicho kwa kukosa gari la kumpeleka kusikiliza kero za wananchi hao.

Katika mkutano huo Bulugu alidai kuwa Mkuu wa Wilaya ya Misungwi alitoa agizo akimtaka Mkurugenzi kufika katika kijiji hicho kufuatia malalamiko yaliyotolewa na wananchi wa Kijiji cha Sanjo kwa kuuomba Uongozi wa Wilaya ya Misungwi ufike hapo kusikiliza kero zao.

Katika taarifa hiyo iliyotengenezwa ili kuwahadaa wananchi wa Kijiji cha Sanjo Bulugu alimsingizia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Misungwi Eliud Mwaiteleke kuwa eti
amekwama kufika katika mkutano huo kutokana na kukosa usafiri kufuatia gari lake kuwepo katika usimamizi wa mitihani ya Taifa kwa wanafunzi wa Darasa la Saba.

“Ndugu zangu wananchi kwa niaba ya Mkurugenzi  napenda kuwaomba radhi kwa kuchelewa kufika hapa mgeni wetu sasa ni saa tano asubuhi ,ni kwamba mgeni wetu hataweza kufika kutokana na kukosa usafiri wa kumleta hapa,gari lake liko kwenye shughuli za Mitihani ya Darasa la saba”alisema Bulugu huku miguno na maswali toka kwa wananchi vikitawala.

“Hivi Mtendaji huoni kuwa huu ni uzembe wa makusudi,magari yote ya Halmashauri hayapo kweli? hata gari lake liko kwenye mitihani?mbona hawa watu wanataka kuturudisha tulikotoka? Sasa tunakuagiza Mtendaji ukamwambie Mkuu wa Wilaya kuwa agizo lake limepuuzwa! kwa nini Mkurugenzi asitumie hata Hiece?” alihoji mmoja wa wananchi waliokuwepo katika mkuitano huo.
Yaliyojiri baada ya Uchunguzi

Uchunguzi uliofanywa kipindi hicho Tanzania Daima lilibaini kuwa, taarifa hizo hazikuwa za kweli kwani Mkurugenzi huyo alikuwa safari ya kikazi Mjini Dodoma.
taarifa hiyo iliwakera wananchi na kuahidi kugomea mikutano ijayo iwapo hawatapata maelezo ya kutosha juu ya tukio hilo ambapo hadi leo hii wananchi hao hawajawahi kusikilizwa kutokana na kwamba mkutano huo ulikuwa kama kiini macho kuficha tuhuma zilizokuwepo kwa watumishi kipindi hicho.

Mwandishi wa Tanzania Daima alimtafuta Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi  ili kutolea ufafanuzi wa taarifa iliyotolewa na Afisa Mtendaji huyo ambapo Mkurugenzi alisema kuwa hazina ukweli.
“Mimi kwa sasa niko Mbeya,nimeshtushwa sana na taarifa hizo mimi nikose usafiri si ningeenda na pikipiki? Sisi kazi yetu ni moja tu nayo ni kuwatumikia wananchi na si vinginevyo sijui Mtendaji huyo kapata wapi maelekezo hayo ngoja nifuatilie”alisema Mwaiteleke.

Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti wananchi hao walisema kuwa wamekwazwa na kitendo cha Mkurugenzi kushindwa kufika kijijini jambo walilosema bila kumung’unya maneno kwamba ni uzembe.

Akiweka wazi siri zilizokuwa zimefichika katika maandalizi ya taarifa za uongo zilizotolewa na Kaimu Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Sanjo Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyasubi Meni Lutandula aliliambia Tanzania Daima  kuwa kuna udanganyifu mkubwa katika ujenzi wa tenki la maji katika kijiji cha Sanjo ambapo walibaini matumizi mabaya ya fedha za wananchi kiasi cha shilingi milioni 20,828,502;60 katika ujenzi wa mradi wa maji.

“Inasikitisha kuna ujenzi wa shule ambayo hata hivyo ilikuwa haijaanza kufanya kazi lakini tayari vyumba vimechakaa kutokana na kujengwa chini ya kiwango wananchi kulazimishwa kuchangia shilingi 6500 kila familia kwa ajiri ya ukarabati wa vyumba hivyo”.alisema Lutandula.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Sanjo Bukali John alipotakiwa kutolea ufafanuzi sakata la ujenzi wa madarasa chini ya kiwango alisema alikiri na kumuonya mwandishi asiripoti taarifa hizo.
“Nisingependa uendelee kufuatilia jambo hilo kwa kuwa wananchi tayari tumeshawashawishi wananchi na wamekubali kuchangia fedha kwa ajiri ya kurekebisha vyumba hivyo ni kweli kuna mapungufu yaliyojitokeza katika ujenzi wa vyumba hivyo lakini sitaki ufuatilie suala hilo maana tayari tumeshafanya vikao na wananchi na tumekubaliana wachangie fedha kiasi cha shilingi 6500 kila familia ili tuweze kukarabati vyumba hivyo” alisema Bukali.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Juma Sweda alipotafutwa kuzungumzia kama alitoa agizo kwa Mkurugenzi ambapo alisema kuwa hana taarifa zozote juu ya agizo hilo na kwamba yeye hajawahi kufanya ziara katika kijiji cha Sanjo.
“Mimi sijawahi kufanya ziara yoyote katika kijiji hicho isipokuwa nilishiriki kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Fela hivyo sijui Afisa Mtendaji huyo alitoa wapi maelekezo hayo nitafuatilia kujua zaidi juu ya jambo hilo”alisema Sweda.
Baraza la Madiwani kuwapa Siku 30 kwa watendaji

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, limewapa muda wa siku 30 watendaji kushughulikia suala la makusanyo ya mapato ya ndani na utekelezaji wa mradi wa maji katika kijiji cha Fela uliokwama tangu 2013.

Azimio hilo lilipitishwa na baraza hilo wakati wa kikao kilichofanyika mjini Misungwi juzi, baada ya kubainika kuwa hadi Desemba 2017 halmashauri hiyo imekusanya Sh734.9 milioni pekee kati ya malengo ya kukusanya Sh2.06 bilioni.

Katika Baraza hilo Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga aliwacharukia watendaji na kuwataka watoe  maelezo juu ya kusuasua kwa ukusanyaji mapato, hali inayokwamisha utekelezaji wa miradi.

Akitolea mfano wa kusuasua alisema kuwa katika mwalo huko Mbarika vitabu vya halmashauri vinaonyesha hakuna mapato yanayokusanywa, lakini hivi karibuni kamati ya uchumi na mipango ilipotembelea eneo hilo ilifanikiwa kukusanya Sh15,000 kwa muda mfupi, hali inayodhihirisha udhaifu katika ukusanyaji wa mapato.

Kuhusu mradi wa maji wa Fella ambao utekelezaji wake ulianza Juni 2013 na kutakiwa kukamilika Desemba mwaka huo, baraza limempa siku 30 mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Eliud Mwaiteleke kuhakikisha unakamilika na kutoa maji au uwekwe chini ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Mradi huo ambao tayari umegharimu zaidi ya Sh644 milioni, unatarajiwa kunufaisha wakazi 6,473 wa vijiji vya Fella, Ngeleka na Bujingwa.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, mhandisi wa maji wa halmashauri hiyo, Ali Mruma alisema tayari maji yameanza kutoka na zinahitajika zaidi ya Sh3.8 milioni kununulia mashine ya kuyasukuma ili kuongeza usambazaji wa huduma kwa wananchi.

Diwani wa viti maalum, Christina Nyanda alisema maji hayo kata ya Mamaye yanatoka kwa kusuasua na kutaka wataalamu kutoa maelezo sahihi.

Mkandarasi wa kampuni ya COWI Tanzania Ltd inayotekeleza mradi huo, Ernest Tinka alikiri kuwapo upungufu na kuahidi kurekebishwa.

Siri zilizofichika nyuma ya miradi Misungwi.

1.      Kuna maslahi binafsi katika utekelezaji wa Miradi mbalimbali Wilayani Misungwi kutokana na baadhi ya viongozi wa Serikali na kisiasa kudaiwa kuwa ndiyo wamiliki wa makampuni yanayotekeleza miradi hiyo ambapo kwa haya aliyokutana nayo Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Suluhisho kuinusuru Miradi ya maendeleo dhidi ya Mchwa.
inatakiwa kuunda Tume Maalumu kwa ajiri ya kuchunguza ufujaji wa mali za Umma lakini pia watumishi wa Wilaya ya Misungwi wahamishwe kutokana na Mtandao wao unaokwamisha kujulikana kwa uozo kupitia kwa Kaimu Afisa Habari wa Wilaya ya Misungwi Thomas Lutego ambaye hata akiwa na shughuli hubagua Waandishi wa Habari kwa lengo la kuficha maovu hayo.
















Wednesday, February 14, 2018

Bundi atua Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu.

Na Antony Sollo Ushetu.
14.feb 2018

MGOGORO mkubwa umeibuka baina ya Emmanuel Makashi ambaye ni Diwani wa Kata na Christopher Rwagasanga Lyogelo ambaye ni Afisa Mtendaji wa Kata ya Sabasabini iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu Mkoni Shinyanga,hali iliyopelekea diwani huyo kuangua kilio katika kikao cha baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo akimtuhumu Afisa mtendaji huyokuhujumu shughuli za maendeleo ya Kata hiyo.

Akiwasilisha malalamiko yake mbele ya Madiwani hao kilichofanyika Februali 14 mwaka huu huko Ushetu Makashi lisema kuwa Afisa Mtendaji huyo amekuwa akibeza kila kitu kinachofanywa na Diwani huyo.

“Mheshimiwa mwenyekiti Afisa Mtendaji huyo amekuwa akichonganisha na wananchi huku akisema kwamba mimi sijasoma,na kuwaambia kuwa yeyendiye anafaa kuwa kiongozi wao akidai kuwa anashahada ya elimu ya juu na kuwaambia kwamba mimi sina uwezo wa kuwaletea maendeleo amekuwa akiwashawishi watendaji wa vijiji kutojishughulisha katika masuala mbalimbali ikiwemo uchangiaji wa shughuli za maendeleo”alisema Makashi.

Kutokana na uchungu aliokuwa nao Makashi aliangua kilio mbele ya viongozi mbalimbali waliohudhuria kikao cha baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichoketi kwa lengo la kujadili mambo mbalimbali ya maendeleo ikiwamo miradi ya maendeleo kwa wananchi wa Ushetu.

Baraza hilo lilihudhuriwa na viongozi mbambli mbali wa Chama na serikali akiwemo mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa pamoja na katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Timoth Ndanya ambapo Diwani huyo aliamua Mtendaji huyo kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga huku akisema.

“Ndugu mwenyekiti kuna tatizo la kiutendaji katika Kata yangu ya Sabasabini kwamba, Afisa Mtendaji wa Kata amekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo kwa wananchi wangu, tangu aanze kazi kwenye Kata yangu mwaka 2016 hakuna maendeleo yoyote kwani amekuwa akiwagomesha wananchi kuchangia shughuli za maendeleo,” alilalamika Makashi.

Katika jitihada za kutatua mgogoro huo Makashi alimuomba Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Matomola Michael kufika katika Kata hiyo ili kuwapatanisha waendelee kuwatumikia wananchi huku akisema tangu kuanza kwa figisu figisu za Afisa Mtendaji huyo hadi sasa hakuna kitu kinachofanyika kutokana na mgogoro huo.

“Mheshimiwa mwenyekiti kibaya zaidi Afisa Mtendaji huyo amekuwa akiwashawishi na watendaji wengine wa vijiji wasinipe ushirikiano katika kutekeleza shughuli za maendeleo kwa wananchi kwa madai kwamba yeye ndiye kiongozi sahihi kutokana na kwamba ana nashahada ya elimu ya juu,kwa kweli nakuomba Mkurugenzi aunde tume ya uchunguzi dhidi yake,kama hutafanya hivyo tubadilishane ofisi wewe uwe diwani na mimi nikae kwenye kiti chako cha ukurugenzi ili na wewe uone vitendo ninavyofanyiwa na Mtendaji huyo,” alisema Makashi kwa uchungu.

Makashi alisema kuwa,kabla ya ujio wa Afisa Mtendaji huyo katika Kata ya sabasabini, kulikuwa na mahusiano mazuri na  wananchi kutokana na ushirikiano mzuri kati yake na kaimu afisa mtendaji aliyekuwapo kipindi cha 2013 /2015 kwa kufanikisha kutimiza agizo la Rais Magufuli juu ya kutengeneza Madawati mashuleni ambapo walifanikisha kuchonga madawati 74 yaliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 8.8

Makashi alisema kuwa katika kipindi hicho alijitolea katika ujenzi wa matundu ya choo cha shule kwa kuchangia kiasi cha shilingi 150,000 na kuongeza kuwa kiasi cha shilingi milioni 5.3 kilitumika kujenga nyumba ya mganga  katika Zahanati ya Kata huku nguvu ya wananchi ni shilingi milioni 1.2.

Makashi alibainisha kuwa katika kipindi cha mwaka 2017 alifanikisha kujenga barabara ya Sabasabini kwenda Iponyang’holo kiwango cha changarawe yenye urefu wa kilometa 9 kwa gharama ya shilingi milioni 2.5 kwa ushirikiano na diwani wake wa viti maalum Felista Nyerere ambaye alichanga shilingi 300,000 kati ya fedha hizo,ambapo alidai kuwa tangu mtendaji huyo aanze kazi shughuli za maendeleo zimesimama kutokana na mgogoro wao.

“Mtendaji huyo alianza kazi katika kata hii tangu mwaka 2016, na alinikuta nikiwa vizuri na wananchi wangu  lakini tangu aanze kazi nimeshindwa kumuelewa labda anaitaka hii Kata!, maana kinachofanywa na Mtendaji huyu ni uvunjaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano na ninaona Mtendaji huyu anapingana na kasi ya Mheshimiwa Rais kwa kuamua kukwamisha shughuli za maendeleo kwa makusudi,mimi naomba Mkurugenzi aunde hiyo Tume ili kuweza kutatua mgogoro huu vinginevyo Kata hii haitaweza kupata maendeleo”alisema Makashi.

Akichangia hoja hiyo Diwani wa Kata ya Bulungwa Joseph Masaluta alilieleza baraza hilo kuwa wote wawili kwa maana ya Diwani pamoja na afisa mtendaji huyo wa Kata wapelekwe kwenye kamati ya maadili kwa lengo la kuhojiwa kwa kina ili kubaini chanzo cha mgogoro wao na kuongeza kuwa wawili hao wamekutana wote ni jeuri.
Katika majibu yake kwa diwani huyo Makamu mwenyekiti wa baraza hilo Gagi Lala ambaye ndiye alikuwa akiongoza baraza hilo alisema,

“Mkurugenzi haiwezekani mtu alalamike kiasi hiki tena hadharani inaonekana kuna tatizo linalopaswa kushughulikiwa, pamoja na kwamba kanuni za baraza haziruhusu kuingiza taarifa zilizo nje ya shughuli za baraza , mheshimiwa diwani ujumbe umefika kuwa mtulivu tutalishughulikia suala hili,” alisema Lala.

Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu Benjamin Onesmo ambaye pia ni afisa maendeleo ya jamii katika Halmashauri hiyo alisema kuwa kutokana na hali hiyo ofisi yake imelichukua suala hilo na italitafutia ufumbuzi wa haraka.
“Mheshimiwa Mwenyekiti ofisi yangu inalibeba suala hilo na litashughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi wa Haraka,” alisema Onesmo”.

MWISHO.

                                                                                                          

Sunday, February 11, 2018

Afisa biashara Manispaa ya Ubungo awaliza mamilioni wafanyabiashara .

Na  Antony  Sollo Ubungo.

AFISA biashara wa Manispaa hiyo Geofry Mbwama anatuhumiwa kujipatia mamilioni ya fedha toka kwa wafanyabiashara wenye maduka pamoja na wajasiriamali katika manispaa hiyo baada ya kuingia kila duka akiomba Leseni ya biashara akiwa na Dereva wa Manispaa hiyo na kufanikiwa kujipatia kiasi kikubwa cha fedha akitumia nyaraka bandia za Serikali Tanzania Daima libaini.

Tukio hilo lilitokea desemba 13 mwaka jana katika Mtaa wa Mbezi Luis Manispaa ya Ubungo Jijini Dar Es Salaam ambapo Mbwama akiwa na gari la Manispa hiyo aliingia katika maduka na vibanda vya wafanyabiashara wadogo mafundi pikipiki hata wanaofanyia shughuli zao nje huku akihoji kama wana Leseni za biashara na pale ambapo alikuta hawana kwa sababu mbalimbali alifunga biashara na makufuli yake na baadaye aliandika nyaraka inayodaiwa kuwa ni feki na kuwapiga faini kati ya 321,000.

Akithibitisha kufanyiwa vitendo hivyo mmoja wa wajasiriamali (Fundi pikipiki) eneo la Mbezi makabe road Rahesh Shaban ambaye anajishughulisha na ufundi wa pikipiki alisema alilazimishwa kufunga shughuli zake baada ya kubainika kuwa hakuwa na leseni ya kufanya kazi ya ufundi licha  ya kujitetea kuwa alikuwa ameenda katika mamlaka ya Mapato Tanzania kwa ajili ya kupatiwa namba ya utambulisho wa mlipa Kodi ( TIN Number) lakini Afisabiashara huyo alimwandikia faini ya shilingi 321,000 na kumwamuru afunge shughuli zake.

“Mimi na wenzangu hapa tumemweleza kuwa tunazo baadhi ya nyaraka na kwamba tayari tulikuwa tumeshaanza mchakato wa kupatiwa namba ya utambulisho ya mlipa kodi( TIN Number) lakini hakutuelewa na matokeo yake aliandika faini katika nyaraka ambazo tunahisi ni feki kwa kuwa nyaraka yoyote ya Serikali huwa haiandikwi kitu chochote au namba ya mtu binafsi ambapo hata hivyo aliomba fedha kiasi kati ya 20,000, mpaka 60,000 tukampatia na hakutoa risiti yoyote”alisema Shabani.

Kwa kuwa Shaban aliona kuwa mahala pale ndipo anapopata riziki kwa ajili ya mahitaji ya familia yake,aliomba asamehewe lakini kilichoshangaza aliombwa shilingi 20,000 na Mbwama lakini hakupatiwa risiti jambo ambalo pia lilithibitishwa na wafanyabiashara wa duka la madawa yaliyoko jirani na Shabani ambao nao walitoa fedha kiasi cha shilingi 60,000 kila mmoja kutokana na kutishiwa kufungiwa maduka yao ambapo fedha hizo zilikabidhiwa kwa dereva wa Manispaa ambaye naye alikuwa akiwakaripia wafanyabiashara na kutoa vitisho vya kuwafungia biashara zao.

Tanzania Daima lilifuatilia nyendo za Mbwama na kukutana na malalamiko lukuki kwamba wafanyabiashara na wajasiriamali wa Mtaa wa Mbezi walio wengi walikuwa wameshachukuliwa fedha zao kutokana na tishio la kufungiwa biashara zao na Afisa biashara huyo akishirikiana na dereva wake.

Mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima alimtafuta Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo ambapo hata hivyo juhudi za kumpata Mkurugenzi huyo ziligonga mwamba kutokana na mwingiliano wa majukumu ambapo lilikutana na Katibu Tawala James Mkumbo ambaye baada ya kupatiwa taarifa juu ya kilichofanywa na watumishi hao dhidi ya wafanyabiashara nawajasiriamali na kuahidi kuzifanyia kazi tuhuma hizo ambapo tangu 13 desemba hadi leo hakuna taarifa zozote.

Mara kadhaa Mkumbo amekuwa akitakiwa kutolea ufafanuzi wa tatizo hilo lakini amekuwa akidai kuwa alikabidhi watu kufanyia kazi tuhuma hizo
“Kwa sasa niko Mwanza lakini kuna watu niliwapa jukumu la kushughulikia suala hilo lakini pia sisi hatufanyi kazi kwa pressure za waandishi wa Habari kwa sababu wanataka habari tukikamilisha utaratibu wetu tutafanya kinachostahili ”alijibu  Mkumbo kwa njia ya ujumbe wa simu ya mkononi.

Kinachoshangaza hapa ni kwamba hakuna taarifa zozote kuhusu ufuatiliaji wa tuhuma hizi pamoja na Katibu Tawala huyo kupelekewa Ofisini tuhuma zinazowakabili Afisa biashara wa Manispaa pamoja na dereva wa Manispaa ya Ubungo kwa takribani miezi miwili sasa jambo linalozua sintofahamu juu ya uadilifu wa watumishi hao

Wananchi waliozungumza na gazeti hili wameiomba Serikali kuwachunguza baadhi ya wafanyakazi wake hasa waliotumbuliwa kwa kuwa sasa wengi wako mtaani hawana kazi na wamegeuka Matapeli wanaotumia mbinu walizokuwa wamezizoea wakiwa kazini kutafuta fedha kwa njia za vitisho na inasemekana Mbwama na dereva wa Manispaa ya Ubungo kwa pamoja wamejipatia mamilioni kwa njia hiyo.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo John Kayombo hakuwez kupatikana mara moja kuzungumzia tuhuma hizo ambapo juhudi za kumtafuta atolee ufafanuzi wa hatua gani zimechukuliwa dhidi ya tuhuma kwa watumishi hao kwa kukiuka maadili ya Utumishi wa Umma

MWISHO.






Friday, February 9, 2018

Wanaume waaswa kutojimilikisha maeneo ya familia



Na Antony Sollo


Februari 9,2018.

WANAUME katika  halmashauri ya mji wa Kahama Mkoani Shinyanga wametakiwa kuachana na dhana ya kujimilikisha  hati miliki za viwanja vyao, ili kutoa  kipaumbele kwa akinamama ili nao waweze kumiliki ardhi   hali ambayo itaepusha migogoro katika familia.

Akizungumza kabla ya kutambulisha mradi wa upimaji wa viwanja 4,000 katika kata ya Mhongolo  afisa ardhi wa halmashauri ya mji wa Kahama   Mashiri Magasa  alisema kuwa wanaume wilayani Kahama wamekuwa na tabia ya kujimilikisha maeneo yote yenye hati miliki  jambo ambalo siyo haki na kwamba hali kama hiyo pindi mwanaume anapofariki dunia humwacha mwanamke katika wakati mgumu.

Magasa  aliyasema hayo februari 8 mwaka huu wakati akizungumza na wananchi wa vitongoji vya sofi, bomani na Nyamhela vilivyoko katika Mtaa wa Mhongolo ambapo aliwaasa wanaume kuachana na dhana ya kujimilikisha maeneo ya familia kwani hali hiyo ndiyo chanzo cha mifarakano katika familia pindi baba wa familia anapoamua kuchukua hati hizo na kuomba mkopo katika taasisi za fedha na kushindwa kurejesha.

“Ifike wakati wanaume muwape fursa ya kumiliki ardhi wanawake kwani kufanya hivyo kunatoa usawa katika familia lakini pia kuna wakati mmoja wa familia hiyo akifariki hasa baba mwanamke hawezi kuhangaika kutokana kuwa tayari anakuwa ana mali halisi inayomfanya aendeleze familia, wanaume wakiachana na mfumo dume mwanamke akashirikishwa ipasavyo katika umiliki huo  hakutakuwepo na migogoro baina yao,” Alisema Magasa.

Katika hatua nyingine Afisa ardhi aliwataka wakazi wa mji wa Kahama kuhakikisha wanapima viwanja vyao kabla ya kufanya ujenzi au shughuli zozote za kimaendeleo na upimaji huo uende sambamba na utafutaji wa hati miliki ili kupunguza migogoro isiyokuwa na tija kwa jamii na kuwafanya waweze kukopesheka kirahisi katika taasisi za fedha.

“Kwa mujibu wa sheria ya Ardhi na mpango miji hakuna mwananchi yoyote hapa nchini anayeruhusiwa kufanya ujenzi wowote wa nyumba za makazi katika kiwanja chake bila ya kupimwa au kujenga nyumba bila ya kufuata ramani za mpango miji tukikuta unajenga kwenye eneo bila kibali tunasitisha ujenzi na kukupiga faini” alisema Magasa.

Kwa mujibu wa mpima ardhi  kutoka kampuni ya  Total Geo survey  Co.Ltd    Emmanuel William   ambaye anayeshughulikia upimaji wa viwanja katika kata hiyo alisema kuwa wananchi wanatakiwa kuchangia  gharama za upimaji ili kazi iweze kuendelea na kwamba mpaka sasa viwanja   4,000 vimepimwa na viwanja 1000 vimepitishwa na  wizara ya ardhi  Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kuwatafutia hati miliki wananchi.

Akizungumzia zoezi hilo William alisema kuwa lengo ni kupima viwanja 12,000 katika Kata hiyo na kuwataka wananchi kuongeza kasi ya kuchangia gharama ya upimaji ambayo ni shilingi elfu tisini 90,000 na kwamba gharama hiyo ni ndogo ukilinganisha na bei elekezi ya serikali ya kuanzia ambayo inaanzia shilingi laki tatu, 3,000,000. Kwa kila kiwanja.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa mtaa wa Mhongolo  Denis  Diocles alisema kuwa lengo la kampuni hiyo ni kupima viwanja elfu 12, lakini viwanja vilivyofikiwa ni 4021, vilivyopewa namba ni 1335, ambavyo havijapewa namba ni 2686 na kutaja mradi wote unagharimu kiasi cha shilingi milioni 361 kati ya hivyo vilivyolipiwa ni 1192 na ambavyo havijalipiwa ni 2828.

Akizungumza katika zoezi la kutamburisha mradi huo Mwenyekiti wa mtaa wa Mhongolo Emmanuel Nangale alisema kuwa kukusanya shilingi milioni 361  kwa wakazi hao siyo kazi ndogo na kudai kuwa kiasi kilichokusanywa hadi sasa kinapswa kupongezwa licha ya watu kutohamasika kikamilifu na kwamba katika halmashauri hiyo ni Mtaa wa Mhongolo pekee umejitutumua katika zoezi hilo.

Mwisho.