Saturday, January 20, 2018

Kushamiri kwa Migogoro ya Ardhi Nchini



Makala:

Zikiwa zimepita siku chache tangu vikao vya Kamati za Bunge vianze mjini Dodoma hali ya mambo katika maeneo mbalimbali nchini si shwari kwani kumezuka mijadala mikubwa kutokana na madhira yaliyowapata wananchi kutokana na kupigwa,kuporwa mali ,kujeruhiwa kwa risasi za moto na Askari wakati wa utekelezaji wa operesheni za kuwaondoa wananchi wanaokaa katika maeneo yanayodaiwa kuwa ni Hifadhi pamoja na Ardhi inayodaiwa kutengwa kwa ajili ya Uwekezaji nk.

Vikao hivyo vilianza jumatatu ya tarehe 15 januari 2018,hii ikiwa ni kabla ya kuanza kwa Mkutano wa kumi wa Bunge,shughuli zilizopangwa kutekelezwa katika kipindi cha vikao hivi ni pamoja na ziara za ufuatiliaji ,uchambuzi wa miswada mbalimbali na kupokea maoni ya wadau pamoja na kupokea taarifa za utendaji za Wizara.

Kamati tatu za kisekta ambazo zitakuwa na jukumu la uchambuzi wa miswada mbalimbali ni pamoja na Kamati ya Sheria,Kamati ya Ardhi,Maliasili na Utalii pamoja na Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Maoni yangu kwa wadau na wajumbe wa Kamati hizi watumie muda huu kuangalia namna ya kutatua tatizo lililomuelemea Mheshimiwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Wiliam Lukuvi ambaye kama angekuwa si Kiongozi Mahiri huenda Rais Magufuli angekuwa ameshamuweka pembeni kutokana na malalamiko likuki yanayoiandama Ofisi (Wizara)yake.

Kipekee niwapongeze Mawaziri hawa wawili Mheshimiwa Wiliam Lukuvi na Naibu wake Mheshimiwa Angelina Mabula kwa kazi kubwa wanayofanya ikiwemo kupokea na kufanyia kazi malalamiko takribani nchi nzima.

Ukweli Wizara hii ni ngumu,ina mianya mingi ya rushwa ambayo kama si umahiri wa Mawaziri hawa huenda Mahakama na Mabaraza ya ardhi kungefurika mafaili ya malalamiko zaidi ya haya,lakini kutokana na uchunguzi nilioufanya naona kabisa na ninaweka bayana kuwa Mawaziri hawa wamejitoa muhanga kwa ajili ya kupigania haki za wananchi wanyonge.


katika mkutano wa tisa wa bunge la kumi na moja November 16, 2017 akijibu maswali ya papo kwa papo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhshimiwa Khasim Majaliwa aliulizwa maswali na wabunge Magdalena Sakaya (Kaliua) aliyetaka kujua Serikali imejipangaje kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi suala ambalo ni la kidunia.

Katika majibu yake Waziri Mkuu alisema,
“Mheshimiwa Spika,mabadiliko ya tabia nchi yaliyokumba dunia na Tanzania ikiwemo,tunaendelea kukabili changamoto kwa  kuweka mipango mbalimbali kuhakikisha kuwa tunakabiliana na mabadiliko hayo,moja ya mikakati hiyo ni kusimamia Sheria ya uhifadhi wa Mazingira ili kuhakikisha Mazingira yanabaki yanasaidia kufanya mabadiliko ya hali ya hewa ya nchi yanabaki kuwa ya kawaida yanayowezesha binadamu au viumbe hai vyote ndani ya nchi kufanya kazi zake vizuri na kupata mahitaji yake vizuri”

Waziri Mkuu pia alisema kuwa Serikali imeendelea kusimamia Sheria za mazingira ambazo pia zinakinga maeneo mbalimbali hii ni pamoja na misitu,mito na maeneo mengine yote ili kukabiliana na hali hiyo.

Serikali pia imeendelea kutoa elimu kwa jamii kuwaelimisha Watanzania umuhimu wa Kutunza mazingira yetu kwa ujumla,zikiwemo taasisi za kimataifa zimeendelea pia kusaidia kupambana na tatizo hili.

Waziri Mkuu alitoa wito kwa watanzania nia wote kutunza mazingira na kwamba mabadiliko ya tabia nchi duniani hayatafanikiwa iwapo tutaendelea kuharibu misitu yetu,kuharibu vyanzo vyetu,tunaweza kukosa huduma za jamii zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi,hivyo ni muhimu sana kushirikiana na wataalamu kwa pamoja na wananchi wanaoishi na kila mmoja aliyepewa dhamana katika maeneo yao ili kuweza kushiriki kwa pamoja kuhifadhi Mazingira yetu.

Waziri Mkuu pia aliulizwa swali na Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale (CUF) kuhusu shambulio lililofanywa julai 2017 na Askari Polisi ndani ya msikiti ambapo shambulio hilo lilipelekea kifo cha Shekh Ismail Weta na kuondolewa jicho kwa Shekh Abdalah Nakindabu ambapo Mbunge huyo alitaka kujua kama Serikali ina mpango wa kulipa fidia  kwa watu hao.

Akijibu swali hilo Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema kuwa kwanza sina uhakika kama Askari walimshambulia mtajwa hapo na kumtoa jicho lakini jukumu la vyombo vya dola na Jeshi la Polisi likiwemo ni kulinda usalama wa raia na mali zao,si jukumu la polisi kwenda kumshambulia mtu na hatimaye Serikali ianze kufikiria kumlipa mtu fidia kutokana na shambulio lililofanywa na Askari Polisi na kama kuna Askari yeyote amefanya tendo hilo yeye mwenyewe nje ya majukumu yake ya kazi atachukuliwa hatua kama yeye aliyetenda kosa hilo.

“Serikali haiwajibiki kulipa fidia ikiwa si sehemu ya maagizo na wala si jukumu la majeshi ya vyombo vya dola bali ikithibitika mmoja kati ya watumishi wa vyombo vya dola ametenda kosa hilo na ikathibitika hivyo,yeye mwenyewe atawajibika kuchukuliwa hatua kali na ili kama kutakuwa na kulipa fidia itakuwa ni moja ya adhabu ambayo itatolewa na vyombo vinavyotoa hukumu”.alisisitiza Waziri Mkuu.

“Kwa hiyo Mheshimiwa Spika niseme tu kwamba,Serikali wala vyombo vyake vya dola havilengi kufanya kazi ya kuwatendea makosa wananchi bali ni kuwalinda wananchi pamoja na mali zao kama tulivyojipanga kufanya kazi”alisema Waziri Mkuu.

 Swali lingine ambalo nimelenga kulitumia kuthibitisha mambo yanayoashiria  kushamiri kwa migogoro ya Ardhi nchini liliulizwa mbele ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Ulyankulu Mheshimiwa Kadutu kuhusu kuzuiwa kwa wananchi kufanya shughuli za kilimo na ufugaji huku maeneo hayo yakiwa yamepimwa na vijiji vyake vimeandikishwa na wananchi wakiwa na (GN) Tangazo la Serikali.

Akijibu swali hilo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Khasim Majaliwa alisema nchi yetu ina mapori yaliyohifadhiwa kisheria,yana mipaka yake rasmi kwa mujibu wa Sheria zinazoyalinda,mapori haya yapo katika kila eneo,na ni budi kila mtanzania kushiriki kuyahifadhi,kumetokea uvamizi unaofanywa na waliojirani na maeneo hayo,ni kweli maeneo hayo yamekuwa na migogoro mingi kati ya mapori yetu na vijiji,kati ya mapori na wananchi ambao wanaoenda kufanya shughuli za kijamii huko ndani ambapo pia Serikali hairuhusu kufanyika kwa shughuli za kijamii.

Kutokana na migogoro hii ya muda mrefu,Waziri Mkuu alitoa agizo kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kufanya mapitio ya mipaka na kuweka alama kwenye mipaka ya mapori yote.

Kilichobainika,Serikali ilikuwa imeshasajili vijiji hivyo na kulianza migogoro hiyo baada ya wataalamu walioanza kwenda kufanya kazi ya kubaini mipaka katika mapori hayo tuliwasihi wananchi walio kwenye vijiji vilivyo ndani ya mapori hayo wawaache wataalamu wafanye mapitio na waweke alama hizo zinazobainisha mipaka ya ramani baada ya hapo Serikali itakuja kuona ni kijiji gani kilicho ndani na je pale palipo kijiji malengo yetu ya uhifadhi yamefikiwa na bado ni Mahitaji sahihi ili baadaye tuje kufanya maamuzi ya au kupunguza maeneo ambayo kwa sasa kwa uhifadhi huo hauna tija ili kuondoa migogoro.

Waziri Mkuu alisema kuwa kazi hiyo inaendelea na aliagiza kuwa ifikapo tarehe 30 mwezi wa kumi na mbili 2017 wataalam hao wawe wamekamilisha kupima mapori ambayo bado  baada ya hapo Serikali iangalie ni vijiji vingapi vilisajiliwa na Serikali na viko ndani ya hifadhi/mapori hayo na kama vijiji hivyo bado viko kwenye maeneo yaliyo na tija kwa malengo ya uhifadhi au la ili Serikali itoe maamuzi mengine.

Waziri Mkuu alitoa wito kwa wananchi ambao wako kwenye hifadhi ambazo zimetambuliwa baada ya uwekaji wa alama uliofanywa na wataalam waendelee na kazi hiyo baada ya kazi hiyo Serikali ifanye mapitio na kufanya maamuzi kwa maslahi ya nchiikiwemo kufuta kijiji au kubadilisha mipaka ambapo mpaka hapo Mahusiano kati ya Serikali na wananchi yatakuwa yameenda vizuri na wananchi watashiriki kulinda mapori na hifadhi hizo.  
Nakubaliana na majibu ya Mheshimiwa Waziri Mkuu Khasim Majaliwa,sasa kero zilizoko katika maeneo mbalimbali Nchini ni namna wahusika walioagizwa kufanya kazi hiyo walivyogeuza zoezi hilo kuwa uwanja wa vita!

Iwapo Serikali imeweza kubaini mapungufu yaliyosababishwa na watendaji mbalimbali wa Serikali katika Taasisi zake kikiwemo Chuo Kikuu cha Dar Es salaam kuingia mikataba vivyo hivyo wapo watendaji wa Serikali walioamua kufanya wanayotaka katika agizo hili la Mheshimiwa Waziri Mkuu hivyo ,kamati ya Maliasili ifuatilie maeneo mbalimbali na maeneo ya kuanza nayo iwe ni Mikoa ya Tabora na Katavi ambapo mpaka hivi sasa vikao vya Kamati za Bunge vinavyoendelea vinaweza kuona ni jinsi gani watendaji wakiwemo wateule wa Mheshimiwa Rais walivyofanya unyama kwa wananchi wa maeneo hayo bila huruma kwa kuchoma vyakula,nyumba,na mali mbalimbali za wananchi jambo linalofanya wananchi waingie mgogoro na Serikali bila sababu.

Kuna aibu kubwa juu ya mambo waliyofanyiwa wananchi kwani wananchi wamefikia hatua za kutozwa fedha kiasi cha shilingi laki moja kabla hata ya utaratibu ulioelezewa vizuri na Mheshimiwa Waziri Mkuu ambapo ingefanyika hivyo,wananchi wasingeweza kupata madhara kiasi cha kusababishwa kwa vifo ,majeruhi,upotevu wa mali na kukosa makazi na aibu ni kwa vijiji vilivyosajiliwa.

Kwa kauli nzuri iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kwamba atambue kuwa viongozi wa Serikali ngazi za chini wamekuwa wakifanya vitu vya kushangaza mpaka wananchi wanajiuliza wana haki gani kwa Serikali yao waliyoiweka madarakani ambapo baada ya muda imekuwa ikiwageuka na kuwaona hawana thamani.

Itambulike kwa ujumla wake kwamba katika zoezi la kuweka mipaka maeneo ya mapori hakukuwa na ushirikishwaji kwa wananchi katika mambo haya ikiwemo matumizi bora ya ardhi haukufanyika hivyo yote yaliyofanyika kuhusu utesaji,uporaji na mengine ilikuwa ni hulka kwa wateule wa Rais ambao walilewa madaraka na kuamua kufanya watakavyo jambo lililosababisha familia za wananchi katika maeneo mbalimbali nchini kuishi maisha magumu ikiwamo kutokuwa na makazi,huduma za kijamii nk.

Nashauri viongozi wakuu wa Kitaifa waweke utaratibu mzuri wa kufuatilia maagizo waliyotoa ili kuona utekelezaji maana pindi wanapoondoka katika maeneo hayo viongozi wa chini yao hugeuka miungu watu na kusahau maelekezo waliyopewa.

MWISHO.




Serikali Yapiga Marufuku Kulima Pamba kwa Mkataba



Zao la Pamba likiwa Shambani picha na Maktaba.
WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali imekataza kilimo cha pamba cha mkataba kwa sababu kinawanyonya wakulima.
Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Ijumaa, Januari 19, 2018) wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua zahanati ya Hunyari wilayani Bunda, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mara.
“Ni marufuku kwa wanunuzi wa pamba kulima pamoja na wakulima kwa sababu wakulima wanakosa uamuzi wa kupanga bei. Kuanzia sasa zao hilo litauzwa kwa njia ya mnada.”
Alisema Serikali imeweka mkakati wa kuimarisha mazao makuu ya biashara ambayo uzalishaji wake umeanza kupungua likiwemo na zao la pamba.
Waziri Mkuu alisema Serikali imeamua kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa kilimo cha zao la pamba kuanzia hatua za maandalizi ya shamba, pembejeo hadi masoko.
Pia Waziri Mkuu amewaagiza Maofisa Kilimo katika wilaya hiyo wawafuate wakulima vijijini kwa ajili ya kutoa elimu itakayowawezesha wakulima kulima kwa kufuata njia bora za kisasa.Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wafugaji kuhakikisha wanakuwa na idadi ya mifugo kulingana na uwezo wa eneo lao.“Marufuku kulisha mifugo katika mashamba ya watu.”
Amesema Serikali itachukua hatua kali za kisheria kwa mfugaji yeyote atakayelisha mifugo yake katika mashamba ya wakulima kwani tabia hiyo huchangia migogo baina yao.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Source: MCHAMBUZI BLOG / 16 minutes ago



Friday, January 19, 2018

HABARI ZA KISIASA ZILIZOTIKISA MWAKA 2017 MKOA WA SHINYANGA


Na Antony Sollo Shinyanga.
Mbwembwe pamoja na ushangiliaji wa aina yake zilivyotawala katika Uchaguzi  ndani ya Chama cha Mapinduzi Mkoani Shinyanga kwa mwaka 2017.

Wahenga walishasema,ukitaka uhondo wa Ngoma ingia ucheze!!!!!!

Hivi ndivyo ilivyokuwa katika uwanja wa siasa ndani ya CCM Mkoani  Shinyanga  ambapo wanachama wa chama hicho walibuni mbinu ya kuhamasisha namna ya kumpata Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoani humo ambapo ilikuwa ni burudani tosha kwa watazamaji wa Uchaguzi wakiwemo waandishi wa Habari.

Kabla ya Uchaguzi na hatua ya kutangaza matokeo ya Uchaguzi ndani ya CCM Mkoani shinyanga kuliibuka mbwembwe na ushangiliaji wa aina yake ambao hautakaa usahaulike.
Mmoja wanachama wa Chama cha Mapinduzi waliotia fola kwa mwaka 2017 ni Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Kiloleli Manyama.
iliyoko Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga 

Diwani huyo  alijizolea umaarufu baada ya kubuni mbinu ya kupiga kampeni akitumia chupa ya chai (Thermos) ambayo ilikuwa imetundikwa katikamoja ya nguzo na kila aliyekuwa akipita aliitikisa na hata kuibusu kama ishara fulani kuonyesha dira na mwelekeo wa mgombea waliyekuwa wameona ataweza kuivusha CCM katika Uchaguzi 2020.

Mwandishi wa Makala hii alifuatilia nini ilikuwa uhalisia juu ya chupa ya chai iliyokuwa imetundikwa kama mtindo mpya wa upigaji kampeni ambapo kupata ufafanuzi huo mwandishi alimtafuta Diwani wa Kata ya Kiloleli ambaye alikuwa na haya ya kuzungumza.
Mwandishi: Mheshimiwa Diwani naomba kufahamu ni kipi kilichopelekea mtundike chupa ya chai katika moja ya nguzo za hema iliyokuwa ndani ya ukumbi wa kupigia kura.

Diwani: ndugu mwandishi,hii ni mbinu mpya tuliyoibuni baada ya kukutana na kukubaliana namna gani tutaweka ishara kwa ajili ya kusaidia upigaji wa kampeni kwa mtu wetu ambaye tunaamini anazo sifa za kuivusha CCM katika chaguzi zijazo ukiwemo wa 2020.
Mwandishi:Mbinu hii imebuniwa na nani?
Diwani: “Mbinu hii nimeiasisi mimi,si unajua siasa ni ushindani na siasa kwa upande mwingine ni ubunifu? Sisi kama wapiga kura baada ya kukaa na kuwapima wagombea wetu walioomba kupigiwa kura tuliona nani atakisaidia chama kukifikisha pale tunapotaka na hasa kwa kuendana na kasi ya Mheshimiwa Rais yaani HAPA KAZI TU”

Mwandishi: kwa hiyo mlikuwa mnapiga kura mkijua ni wapi na ni nani anayeshinda?
Diwani: Hapana! Kutokana na mfumo wa Demokrasia,kila mtu anayo haki ya kuchagua mtu au kiongozi anayemtaka hivyo baada ya kupiga kampeni nikiwapa wazo langu wanachama kwa ujumla wao,tulikubaliana kuwa kwa wale watakaokuwa tayari kuniunga mkono juu ya maoni na mawazo yangu ishara kubwa ni kufika na kuibusu na kuitikisa chupa hiyo na ndiyo kilichotokea na baada ya kuona watu wengi wakipita na kuibusu na kuitikisa chupa niliona wazo langu limekubalika na jambo hili lilinifanya nielewe kuwa kazi ya hamasa niliyoifanya ilikuwa imezaa matunda!

Kutokana na uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala hii, Diwani wa Kata ya Kiloleli Manyama ameweza kuwa mwanasiasa wa mwaka 2017 aliyebuni mbinu ya kuweza kupata matokeo ya kile alichokibuni na kushinda kabla ya kutangazwa kwa matokeo jambo ambalo wengi hata wale ambao wanaweza kuhonga ili wapigiwe kura imekuwa vigumu kujua nai kampigia kura na nani hakumpigia kura mpaka baada ya matokeo ndipo wanapokuja kupata matokeo.

Katika Uchaguzi huo uliofanyika Desemba 5, 2017 katika uwanja wa CCM Kambarage Mjini Shinyanga,Mabala Mlolwa aliibuka kidedea baada ya kuwabwaga washindani wake ambapo Mlolwa alipata kura 702  John Festo Makune kura 35 na Cornel Ngudungi  akiambulia kura 02.

Msimamizi wa uchaguzi na mlezi wa Chama hicho Mkoani Shinyanga Abdallah Juma Magodi  ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar alimtangaza Mabala Mlolwa kuwa ndiye mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga.

“Naomba kusoma matokeo ya kazi tuliyoifanya,Ndugu Mabala Mlolwa kura 702  Ndugu John Festo Makune kura 35 na Cornel Ngudungi kura 02.
“Hivyo kwa mamlaka niliyopewa ya kuwa msimamizi wa Uchaguzi huu namtangaza ndugu Mabala Mlolwa kuwa ndiye Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga.”alisema Abdallah.

Kwa nafasi ya mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ikichukuliwa na Gaspar Kileo  aliyepata kura 702 dhidi ya wapinzani wake Bernad Shigela aliyepata  kura 33 na
Joyce Masunga-02.







  
Wajumbe wakiwa wanaendelea na zoezi la upigaji kura katika ukumbi wa Uwanja wa Kambarage Mkoani Shinyanga.Picha na Antony Sollo

 Diwani wa Kata ya Kiloleli Mh Manyama akiwa na Diwani wa Viti Maalumu pamoja na Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mh Suleiman Nchambi mwenye fimbo wakijadili jambo wakiwa na chupa ya chai iliyokuwa ndiyo kivutio cha wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga wakiwa kwenye Uchaguzi wa chama hicho Uwanja wa Kambarage Mkoani Shinyanga. Picha na Antony Sollo.








Mwenyekiti wa  CCM Mkoa wa Shinyanga  Mabala Mlolwa akiomba kura kwa wajumbe ili wampigie kura  kwa nafasi aliyoomba kuwa Mwenyekiti wa Chama Mkoa wa Shinyanga:  Picha na Antony Sollo



Mjumbe wa NEC Mkoa wa Shinyanga Mh Gasper Kileo akiwa na wajumbe wa Chama Mkoa waShinyanga kabla ya kujiuzuru kwa ajili ya kufanyika kwa uchaguzi -  Picha na Antony Sollo 



 Wajumbe wa Mkutano Mkuu wakiendelea na zoezi la kupiga kura katika ukumbi wa Mkutano uliofanyika ndani ya uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga Picha na Antony Sollo

 Mh Manyama Diwani wa Kata ya Kiloleli akionyesha ishara ya kunywa maziwa ikiwa ni ishara ya ushindi baada ya kuasisi mbinu mpya ya upigaji wa kampeni mbinu iliyovutia wengi.


 Maballa Mlolwa akiwa na wagombea  wa nafasi mbalimbali kabla ya Uchaguzi wa nafasi ya Mwenyekiti ambapo aliibuka kidedea na kufanikiwa kuishikilia nafasi ya Mwenyekiti wa Mkoa wa Shinyanga Picha na Antony Sollo

Mwenyekiti wa  CCM Mkoa wa Shinyanga  Mabala Mlolwa akitoa neno la shukrani kwa wajumbe walimpigia kura baada ya kuibuka mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoani Shinyanaga:  Picha na Antony Sollo

MWISHO.

Kwa Taarifa Matukio mbalimbali pamoja na matangazo wasiliana na Katibu wa TAMRA kwa namba 0762 116 116/ 0762 117 117/ 0785 118 118.
antonysollo5@gmail.com