Na antony Sollo Geita
07.09.2017
MFANYABIASHARA Ernest Nyororo mkazi wa Geita analalamikiwa
na wananchi kwa uchafuzi wa Mazingira ikiwemo kuathiri Afya za wananchi kutokana na kusimika mashine za kusaga na kukoboa
mpunga katika maeneo ya makazi ya watu
na kusababisha mvutano na viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Moringe Tanzania
Daima limeelezwa.
Akizungumza na Tanzania Daima Mwenyekiti wa Mtaa wa
Moringe Adriano Rwechungura alisema kuwa Ofisi yake imejitahidi kusuluhisha
jambo hili kwa kuiandikia barua Ofisi ya Mkurugenzi wa Mtendaji wa Mji wa Geita
bila mafanikio ambapo hata hivyo walichukua hatua ya kumuandikia Mratbu wa NEMC
Kanda ya Ziwa kwa hatua zaidi kwa madai kwamba Nyororo anatumia fedha zake kama
fimbo ya kuwanyanyasa wananchi wanyonge.
“Sisi tumechukua hatua ya kumuandikia Mratibu wa NEMC
Kanda ya Ziwa kutokana na jeuri ya mwekezaji huyu maana anatumia fedha zake
vibaya kwamba tumeandika barua zaidi ya mara tano lakini hatuoni mabadiliko
yoyote ambapo tumeona kila maafisa wanapoenda pale wananyamazishwa kwa fedha
hatimaye tukachukua hatua hii”alisema Rwechungura
Tanzania Daima limepata nakala ya barua ya malalamiko
yenye kumb Na NEMC/MZA/CMP/VOL1/49 iliyoandikwa na Mratibu wa baraza la
Mazingira Kanda ya Ziwa kwenda kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa
Geita ya tarehe 13/12/2016 ikikiri kupokea barua ya malalamiko kuhusu kero ya
vumbi inayotokana na Mashine za kusaga na kukoboa mali ya Ernest Nyororo makazi
wa Geita.
Katika barua hiyo,Mratibu wa NEMC Kanda ya Ziwa Jamal
Baruti anamuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Geita
kushughulikia kisheria suala hilo kwa kutumia kanuni na taratibu za Mazingira Mipango
miji na Afya.
“Tunaomba suala hili lishughulikiwe kulingana na
Sheria kanuni na taratibu za Mazingira Mipango miji na Afya kwani tunaamini
kwamba utatuzi wa jambo hili ko ndani ya mamlaka ya Halmashauri”ilisema sehemu
ya barua hiyo.
Kwa mujibu wa Kanuni na taratibu za Mazingira Maafisa
wa Mazingira wa Wilaya na Miji wanayo mamlaka kamili ya kuhakikisha Sheria ya
Mazingira ya 2004 inasimamiwa na kutekelezwa ipasavyo,aidha Maafisa
wanaosimamia mipango miji na masuala ya Afya wanayo pia mamlaka ya kuhakikisha
Sheria husika zinasimamiwa na kutekelezwa.
Hata hivyo Gazeti hili lilimtafuta Ernest Nyororo
kuzungumzia mgogoro huo ambapo alikana na kusema kuna msuguano mkali dhidi yake
na mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Moringe Adriano Rwechungura ambaye Nyororo alidai kuwa
Mwenyekiti huyo anatumia njia za kifisadi kutaka kumchafua.
“mimi sijakaidi maelekezo ya baraza la Mazingira
isipokuwa kuna tatizo kubwa la kutokuwepo kwa maelewano na Mwenyekiti wa
Serikali ya Mtaa Adriano Rwechungura amejificha nyuma ya jirani yangu ambaye
hata hivyo nilipopewa maelekezo na watu wa NEMC kuziba mabati hapo kwenye eneo
langu ndivyo nilivyofanya je walitaka nifanye nini zaidi?alihoji Nyororo.
Kwa upande wake Afisa wa Mazingira wa Halmashauri ya
Mji wa Geita aliyefamika kwa jina moja la Shwekelela alipotafutwa kuzungumzia
sakata hilo alisema yuko nje na Ofisi hivyo kuahidi atafutwe siku nyingine
ambapo Tanzania Daima lilimtafuta tena kupitia namba ya mkononi 0785 909 308 ambapo
simu hiyo iliita bila majibu na juhudi za kumtafuta zinaendelea.
MWISHO