Na Antony Sollo Ushetu.
14.feb 2018
MGOGORO mkubwa umeibuka baina ya Emmanuel Makashi ambaye
ni Diwani wa Kata na Christopher Rwagasanga Lyogelo ambaye ni Afisa Mtendaji wa
Kata ya Sabasabini iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu Mkoni Shinyanga,hali
iliyopelekea diwani huyo kuangua kilio katika kikao cha baraza la Madiwani wa
Halmashauri hiyo akimtuhumu Afisa mtendaji huyokuhujumu shughuli za maendeleo
ya Kata hiyo.
Akiwasilisha malalamiko yake mbele ya Madiwani hao kilichofanyika
Februali 14 mwaka huu huko Ushetu Makashi lisema kuwa Afisa Mtendaji huyo
amekuwa akibeza kila kitu kinachofanywa na Diwani huyo.
“Mheshimiwa mwenyekiti Afisa Mtendaji huyo amekuwa akichonganisha
na wananchi huku akisema kwamba mimi sijasoma,na kuwaambia kuwa yeyendiye
anafaa kuwa kiongozi wao akidai kuwa anashahada ya elimu ya juu na kuwaambia kwamba
mimi sina uwezo wa kuwaletea maendeleo amekuwa akiwashawishi watendaji wa vijiji
kutojishughulisha katika masuala mbalimbali ikiwemo uchangiaji wa shughuli za maendeleo”alisema
Makashi.
Kutokana na uchungu aliokuwa nao Makashi aliangua
kilio mbele ya viongozi mbalimbali waliohudhuria kikao cha baraza la Madiwani
wa Halmashauri hiyo kilichoketi kwa lengo la kujadili mambo mbalimbali ya
maendeleo ikiwamo miradi ya maendeleo kwa wananchi wa Ushetu.
Baraza hilo lilihudhuriwa na viongozi mbambli mbali wa
Chama na serikali akiwemo mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa
pamoja na katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Timoth Ndanya ambapo Diwani huyo
aliamua Mtendaji huyo kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga huku akisema.
“Ndugu mwenyekiti kuna tatizo la kiutendaji katika Kata
yangu ya Sabasabini kwamba, Afisa Mtendaji wa Kata amekuwa kikwazo kikubwa cha
maendeleo kwa wananchi wangu, tangu aanze kazi kwenye Kata yangu mwaka 2016
hakuna maendeleo yoyote kwani amekuwa akiwagomesha wananchi kuchangia shughuli
za maendeleo,” alilalamika Makashi.
Katika jitihada za kutatua mgogoro huo Makashi
alimuomba Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Matomola Michael kufika
katika Kata hiyo ili kuwapatanisha waendelee kuwatumikia wananchi huku akisema
tangu kuanza kwa figisu figisu za Afisa Mtendaji huyo hadi sasa hakuna kitu kinachofanyika
kutokana na mgogoro huo.
“Mheshimiwa mwenyekiti kibaya zaidi Afisa Mtendaji huyo
amekuwa akiwashawishi na watendaji wengine wa vijiji wasinipe ushirikiano
katika kutekeleza shughuli za maendeleo kwa wananchi kwa madai kwamba yeye
ndiye kiongozi sahihi kutokana na kwamba ana nashahada ya elimu ya juu,kwa
kweli nakuomba Mkurugenzi aunde tume ya uchunguzi dhidi yake,kama hutafanya
hivyo tubadilishane ofisi wewe uwe diwani na mimi nikae kwenye kiti chako cha
ukurugenzi ili na wewe uone vitendo ninavyofanyiwa na Mtendaji huyo,” alisema
Makashi kwa uchungu.
Makashi alisema kuwa,kabla ya ujio wa Afisa Mtendaji huyo
katika Kata ya sabasabini, kulikuwa na mahusiano mazuri na wananchi kutokana na ushirikiano mzuri kati
yake na kaimu afisa mtendaji aliyekuwapo kipindi cha 2013 /2015 kwa kufanikisha
kutimiza agizo la Rais Magufuli juu ya kutengeneza Madawati mashuleni ambapo
walifanikisha kuchonga madawati 74 yaliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 8.8
Makashi alisema kuwa katika kipindi hicho alijitolea katika
ujenzi wa matundu ya choo cha shule kwa kuchangia kiasi cha shilingi 150,000 na
kuongeza kuwa kiasi cha shilingi milioni 5.3 kilitumika kujenga nyumba ya
mganga katika Zahanati ya Kata huku nguvu ya wananchi ni shilingi milioni
1.2.
Makashi alibainisha kuwa katika kipindi cha mwaka 2017
alifanikisha kujenga barabara ya Sabasabini kwenda Iponyang’holo kiwango cha
changarawe yenye urefu wa kilometa 9 kwa gharama ya shilingi milioni 2.5 kwa
ushirikiano na diwani wake wa viti maalum Felista Nyerere ambaye alichanga
shilingi 300,000 kati ya fedha hizo,ambapo alidai kuwa tangu mtendaji huyo
aanze kazi shughuli za maendeleo zimesimama kutokana na mgogoro wao.
“Mtendaji huyo alianza kazi katika kata hii tangu
mwaka 2016, na alinikuta nikiwa vizuri na wananchi wangu lakini tangu
aanze kazi nimeshindwa kumuelewa labda anaitaka hii Kata!, maana kinachofanywa
na Mtendaji huyu ni uvunjaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano na ninaona
Mtendaji huyu anapingana na kasi ya Mheshimiwa Rais kwa kuamua kukwamisha shughuli
za maendeleo kwa makusudi,mimi naomba Mkurugenzi aunde hiyo Tume ili kuweza
kutatua mgogoro huu vinginevyo Kata hii haitaweza kupata maendeleo”alisema
Makashi.
Akichangia hoja hiyo Diwani wa Kata ya Bulungwa Joseph
Masaluta alilieleza baraza hilo kuwa wote wawili kwa maana ya Diwani pamoja na
afisa mtendaji huyo wa Kata wapelekwe kwenye kamati ya maadili kwa lengo la
kuhojiwa kwa kina ili kubaini chanzo cha mgogoro wao na kuongeza kuwa wawili
hao wamekutana wote ni jeuri.
Katika majibu yake kwa diwani huyo Makamu mwenyekiti
wa baraza hilo Gagi Lala ambaye ndiye alikuwa akiongoza baraza hilo alisema,
“Mkurugenzi haiwezekani mtu alalamike kiasi hiki tena
hadharani inaonekana kuna tatizo linalopaswa kushughulikiwa, pamoja na kwamba kanuni
za baraza haziruhusu kuingiza taarifa zilizo nje ya shughuli za baraza ,
mheshimiwa diwani ujumbe umefika kuwa mtulivu tutalishughulikia suala hili,”
alisema Lala.
Kwa upande wake kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu Benjamin Onesmo ambaye pia ni afisa maendeleo
ya jamii katika Halmashauri hiyo alisema kuwa kutokana na hali hiyo ofisi yake
imelichukua suala hilo na italitafutia ufumbuzi wa haraka.
“Mheshimiwa Mwenyekiti ofisi yangu inalibeba suala
hilo na litashughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi wa Haraka,” alisema Onesmo”.
MWISHO.