Saturday, September 9, 2017

Wananchi Maganzo waiponda Kamati ya Ndugai.



·        Wasema iliacha kuangalia matatizo ya wananchi
·        Ilienda kwa ajili ya kuangalia madini pekee.
·        Wasema huo si uzalendo,Utaifa.
·        Kamati hiyo haikufanyi kazi Mgodi wa Elhilal ulioko hapo

Na Antony Sollo Shinyanga.
09.09.2017

WANANCHI wa Mji mdogo wa Maganzo Wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga wametoa maoni yao kuhusu ripoti iliyowasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli huku wakiiponda Kamati iliyoundwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai wakisema Kamati hiyo ina mapungufu makubwa Tanzania Daima limeelezwa.

Akizungumza na gazeti hili mmoja wa wahanga wa mgodi huo George Joseph ambaye alipigwa risasi na walinzi wa mgodi huo ameilalamikia Kamati hiyo kwa kushindwa kuangalia maisha ya Raia na badala yake Kamati hiyo imedaiwa kujikita zaidi kuangalia wizi wa Madini ya Almasi katika Mgodi mmoja huku Mgodi unaomilikiwa na Phantom ambaye anamiliki Kampuni ijulikanayo kama Elhilal Mining ukiachwa bila kuchukuliwa taarifa zake yakiwemo mauaji ya wananchi wakazi wa Maganzo.

“ Ripoti ya Kamati hii ina mapungufu makubwa sana kwani ujio wake haukulenga kukutana na wahanga na pia ilipata makengeza kwa kushindwa kuuona mgodi wa Elhilal Mining unomilikiwa na Pantom ambapo Kamati hiyo imekutana na watu ambao taarifa zao zimejikita kwenye madini pekee lakini haikukumbuka kama kuna matukio makubwa ya Mauaji, unyanyasaji wa raia kama ilivyokuwa katika Kamati iliyoundwa kuchunguza zoezi la Operation Tokomeza ambapo Kamati hiyo ilizama zaidi katika masuala ya Haki za Binadamu kujua matatizo yiyowapata raia”alisema George.

George ameeleza kusikitishwa kwake na ubaguzi uliofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Nyabaganga Talaba kwa kuwazuia waathirika waliopigwa risasi na walinzi wa Mgodi wa Mwadui kuingia katika kikao cha Kamati hiyo ili kueleza hali halisi na yanayojili kila siku katika Mgodi wa Mwadui na kwamba eneo la Mgodi wa Mwadui halimilikiwi na WDL pekee bali kuna mwekezaji mwingine ambaye amekuwa tishio kwa usalama wa raia kutokana na kuua vijana wengi na haku akilindwa na viongozi wa Serikali na hadi sasa hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi yake.

“Mwekezaji huyu ameua watu wengi na viongozi wa Jeshi la Polisi na Madaktari waliokuwepo kipindi cha awamu ya Nne walikuwa na mnyororo mkubwa wa rushwa ambapo vijana wengi waliuawa na kupelekwa gerezani huku mmiliki wa Kampuni ya Elhilal akishinikiza vijana wanaokamatwa kupelekwa gerezani na kuwekwa mahabusu kwa lengo la kutukomoa,Phantom amediliki kunyang’anya maeneo ya watu lakini Serikali ilikuwa imewekwa mfukoni hebu tumuombe Mh Rais aje tumweleze mateso tuliyo nayo sisi wananchi wa Maganzo”alisema George.

Kwa mujibu wa George Joseph ambaye ni mmoja wa waathirika kutokana na kupigwa risasi na walinzi wa mgodi wa Mwadui  ni kwamba kuna makundi mbalimbali yaliyoachwa kusikilizwa na Kamati ya Ndugai na bila kuyataja makundi hayo ripoti hiyo inakuwa haijakamilika na inakuwa na doa lisilofutika.

Uchunguzi uliofanywa na Mwandishi wa gazeti hili umebaini kuwa Kamati hiyo ilipata kigugumizi cha kukutana na wahanga waliopata ulemavu kutokana na kushambuliwa kwa risasi za moto na walinzi wa Kampuni ya Zenity Security inayolinda rasrimali za mgodi wa Mwadui pamoja na walinzi wa Kampuni ya Elhilal Mining ambapo baada ya kulalamika sana wahanga hao waliahidiwa na Kamati hiyo kwamba wangekutana na Wajumbe wa Kamati hiyo Mjini Dodoma kabla ya kukabidhi Ripoti kwa Rais John Pombe Magufuli na sasa wanajiuliza! kwa kuwa Kamati hiyo imekabidhi ripoti hiyo bila kuwasikiliza watapata wapi tena nafasi ya kukutana ili waweze kueleza matatizo yao?


Katika hatua nyingine George na wenzake wamemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya uchunguzi wa Viongozi wa Jeshi la Polisi waliokaa muda mrefu Mkoani Shinyanga maana kuna taarifa za kuwepo kwa namna Fulani ya ushirikiano kati ya taasisi za Serikali na Makampuni yanayofanya shughuli zake katika eneo la Mwadui.

“ kuna kesi nyingi za mauaji,kujeruhi kwa silaha za moto zimekuwa zikizimwa muda mrefu kwa ushirikiano wa madaktari wa Hospitali ya Serikali wakati wa uchunguzi wa majeruhi zikiwemo maiti baada ya mauaji yanayotokana na walinzi wa mgodi wa Mwadui na Elhilal inayomilikiwa na Phantom”.alisema George.

Ameyataja makundi hayo kama ifuatavyo.

Waliopigwa risasi na kupata ulemavu wa kudumu.

Katika kundi hili George anasema liko na watu wafuatao, yeye mwenyewe George Joseph Bwisige (alipigwa risasi na kupelekea kukatwa mguu wa kulia lakini hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa),Hamud Said , Marco Ngussa (ambaye alipigwa risasi na kupasuliwa bandama),Nyalulu Sitta (alipigwa risasi na kutobolewa jicho),

Kundi lingine ni la watu waliouawa kwa kupigwa risasi na Askari wa mgodi.

Hawa ni Benard Edward maarufu (Mayo), Shilagi Masali mkazi wa Masagala,Jishosha Daud, Hamad Shunda Mkazi wa Ikonongo ambaye hakuonekana isipokuwa nguo zake pekee tu ndiyo zilizoonekana

Hawa ni kundi dogo tu ambao taarifa zao zimeweza kupatikana na wengi wamepotelea katika mashimo yenye kina kirefu baad ya kukimbizwa wakielekezwa huko kwa lengo la kuwaua na wanamuomba Rais Magufuli aweze kuangalia utaratibu unaofaa ili kuwapatia kifut jasho waweze kukidhi mahitaji ya kibinadamu maana wamefanyiwa ukatili usiowezakusahaulika maishani mwao.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekabidhiwa Ripoti Maalumu ya kuchunguza Biashara ya Madini ya Almasi na Tanzanite nchini 7 Agosti 2017 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa tukio lililofanyika katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam.

Kabla ya kukabidhiwa Ripoti hizo  kwa Rais Magufuli na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai alizipokea ripoti hizo kutoka kwa Wenyeviti wa Kamati Maalumu alizoziunda ambazo zilijumuisha Wabunge wa Bunge la Tanzania kutoka vyama mbalimbali vya Siasa.

Kamati hizo ziliongozwa na Dotto Biteko aliyeongoza Kamati ya kuchunguza biashara ya Madini ya Tanzanite na Mussa Azzan Zungu Kamati ya kuchunguza biashara za Madini ya Almas.

 Kamati hizo ziliundwa wakati wa Mkutano wa Saba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kuchunguza mfumo bora wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa biashara ya madini ya Almas na Tanzanite.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa ripoti hizo, Rais Magufuli amemtaka Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwaita Wataalamu na Taasisi zote zinazohusika na masuala ya madini kufanya maandalizi ya kubadili Sheria zitakazosaidia Taifa kunufaika na rasilimali zake za madini.

 “ Huu ndiyo wakati wa kubadilisha sheria zetu. Mhe, Waziri Mkuu uwaite Wataalam wote wanaohusika na madini maandalizi haya yaanze haraka,” amesema Dkt. Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amesisitiza suala la uzalendo kwa Watanzania wote katika kusimamia rasilimali za nchi na kusema kuwa, ikiwa watanzania wataweka mbele uzalendo Taifa litasimama na kwamba hatutochezewa na wawekezaji tena na mikataba mibovu ambayo italiingizia Taif letu hasara.

Dkt. Magufuli amesema hivi sasa uchumi wa Tanzania unakua kwa asilimia 7 hadi 7.1 na nchi ya nne nyuma ya nchi ya Ethiopia ambayo uchumi wake unakua kwa asilimia 8.3 na kueleza kuwa, iwapo rasilimali hizo zingesimamiwa vizuri taifa lingenufaika zaidi na kuwa na uchumi zaidi ya nchi ya India ambayo haizalishi madini ya Tanzanite lakini imekuwa ni muuzaji mkubwa wa madini hayo.

 “ Tutangulize maslahi ya nchi yetu mbele,nataka tufike mahali tuanze upya,Mhe. Spika muendelee kutusaidia katika kusimamia rasilimali zetu, amesema Dkt. Magufuli.”

Katika hatua nyingine Rais Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Wateule waliotajwa katika ripoti hiyo kukaa pembeni ili kupisha vyombo vya Ulinzi na Usalama kufanya kazi yake vizuri.

Rais Magufuli amesema hayo yote yanafanyika ili kuh akikisha kwamba watanzania wananufaika na rasilimali hizo na kueleza kuwa, bado watanzania hawajanuifa vya kutosha na rasilimali za nchi ikilinganishwa na rasilimali zilizopo.

Awali, akizungumza wakati wa kukabidhi Ripoti hizo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema kuwa, Kamati mbili zilizoundwa na Spika wa Bunge zimefanya kazi kubwa na hali hiyo inatokana nia ya dhati aliyoionyesha Rais Magufuli kuhakikisha,rasilimali za madini zinakuwa na tija kwa Taifa.

 Kwa upande wake Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai alisema kuwa, Bunge liko tayari kuzipitia na kuzifanyia marekebisho Sheria zote ambazo hazilinufaishi Taifa na kueleza kuwa ipo haja ya kulifanyia kazi suala la mifumo ya udhibiti wa rasilimali hizo.

Ndugai amewataka viongozi wa Serikali waliopewa dhamana ya kusimamia shughuli za Umma kuguswa na umaskini wa Watanzania na hivyo kuzitaka Bodi mbalimbali nchini kubadilika na kuona haja ya kuangalia na kufuatilia kwa karibu maeneo wanayoyasimamia.

Akiwasilisha ripoti ya Madini ya Almasi Mwenyekiti wa Kamati hiyo  Mussa Azzan Zungu alisema soko la madini ya Almasi bado liko katika kiwango duni japokuwa Almas yenye thamani ya juu inapatikana Tanzania pekee.
a
 Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Tanzanite Dotto Biteko alieleza kuwa, asilimia 80 ya Tanzanite inatoroshwa nchini na asilimia 20 ya madini hayo ndiyo yanayoingia katika mfumo wa kodi nchini.


MWISHO.

Friday, September 8, 2017

Wachungaji wa Makanisa wadaiwa kuvamia Eneo la Shule


Na Antony Sollo Geita

Wachungaji wa Makanisa ya Grory of God, PVTC , CGT yaliyoko Mtaa wa Moringe Kata ya Buhalahala Mkoani Geita wameingia katika mvutano mkali na Uongozi wa Serikali ya Mtaa huo wakidaiwa kuvamia maeneo ya Shule ya awali ya Moringe Tanzania Daima linaweza kuripoti.

Licha ya Viongozi wa Makanisa hayo kuamuriwa kuondoka katika maeneo hayo na Mratibu wa baraza la Mazingira NEMC kutoka Halmashauri ya Mji wa Geita,Utekelezaji wa amri hiyo umekuwa ni mgumu kutokana na wachungaji hao kukaidi amri hiyo ambapo kanisa lililokuwa limeezekwa kwa maturubai sasa limeezekwa kwa kasi kwa kutumia bati.

Akizunguma na Tanzania Daima Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Moringe Adriano Rwechungura alisema kuwa,Viongozi hao wamekuwa wakiombwa mara kadhaa kuhama na kutafuta maeneo yanayofaa kwa kuendesha ibada zao lakini wameshindwa kuheshimu taratibu za Serikali na kuendeleza malumbano makubwa ambapo hadi sasa kuna mvutano mkubwa kati ya Serikali na taasisi hizo.

“Tumekuwa tukiwasihi viongozi hao wa Makanisa wafuate taratibu zilizowekwa na Serikali lakini hawataki na ni kwamba uwepo wa Makanisa katika eneo la Shule hiyo ni uvunjaji wa Sheria na ukwamishaji wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu kwani kumekuwa na kelele nyingi zinazotokana na ibada zinazofanywa na waumini hao”alisema Rwechungura.

Kwa upande wake Msimamizi wa Shule ya awali ya Moringe Mwalimu Msafiri Masolwa alikiri kuwepo kwa kero katika eneo la Shule hiyo  na kusema kuwa Serikali itafakari juu ya mwingiliano wa taasisi hizo iwapo Shule au kanisa ibaki katika eneo hilo kufuatana na uhitaji wa wananchi wenyewe .

‘Taratibu ziangaliwe kwamba ni taasisi ipi ilikuwa ya kwanza kuanzisha shughuli zake katika eneo hilo na iwapo shule itaonekana ilikuwa ya kwanza ibaki na kama Kanisa lilikuwa la kwanza kuwepo katika eneo hilo basi hakuna budi kubakia katika eneo hilo alisema Masolwa”

Akizungumza na gazeti hili Katibu wa Tawi la Moringe kupitia Chama cha Mapiduzi Robert Maganga alisema kuwa katika  kulifuatilia suala wamekutana na mratibu wa baraza la Mazingira Mkoa wa Geita na kuambiwa kuwa,viongozi hao waliamuriwa kuondoka katika maeneo ya shule hiyo ndani ya siku saba lakini utekelezaji hujafanyika hadi sasa.

Kwa Mujibu wa  Rwechungura Wengine walioingia mgogoro na Serikali ya Mtaa wa Moringe ni pamoja na familia nne ambazo ziko katika eneo la Shule hiyo na kwamba zilishapewa notsi ya kupisha eneo la Shule na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita lakini wanafamilia hao walikataa kufanyiwa tathimini na kwamba Ofisi ya Mwenyekiti wa Mtaa inasubiri Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita atoe notsi kwa mara ya pili.

Kuhusu ujenzi wa barabara za Mtaa, Mwenyekiti wa Mtaa wa Moringe Adriano Rwechungura alimtuhumu Diwani wa Kata ya Buhalahala Elias Kabese kwa kuhujumu miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mtaa wake.



“Diwani wetu hajatutendea haki kwani amehujumu miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara kwamba March 2017 zilitolewa fedha za mfuko wa jimbo  na Mbunge wetu Mheshimiwa Costantine Kanyasu  kiasi cha shilingi mil 4 ambazo zilipangwa kwa ajili kuchongewa barabara kila Mtaa kwa masaa 8 lakini Diwani kwa sababu anazozijua yeye ameutenga Mtaa wetu na hadi sasa hakuna barabara hata moja iliyochongwa kupitia fedha za mfuko wa Jimbo zilizotolewa na Mbunge wetu na kwamba kufuatia hali hiyo ya kibaguzi iliyoonyeshwa na Diwani huyo wananchi wakazi wa Mtaa wa Moringe wameamua kuchangishana wenyewe na kwamba  Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita imekubali kutoa Greda  kwa ajili ya kuchonga barabara za Mtaa”.alisema Rwechungura.

Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini Costantine Kanyasu alipotafutwa na Mwandishi wa gazeti hili ili kuzungumzia fedha za mfuko wa Jimbo alizotoa na tuhuma za ubaguzi unaofanywa na Diwani wa Kata ya Buhalahala Kanyasu likiri kutoa fedha hizo kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Mtaa, lakini Mbunge huyo alionyesha wasiwasi wake kuhusu uadilifu wa Diwani huyo.

“ Usishangae ukisikia fedha hizo hazijafanya kazi iliyokusudiwa maana huyo bwana mdogo ni mjanjamjanja sana,sina uhakika kuhusu matumizi ya fedha hizo lakini kufuatia malalamiko hayo tutafanya utaratibu katika vikao vyetu vya halmashauri na ikibidi tutamtuma Mkaguzi wa ndani ili kwenda kujiridhisha juu ya matumizi ya fedha hizo na ikibainika kuwa kulikuwa na matumizi tofauti na malengo ya kutolewa kwa fedha hizo hatua stahiki zitachukuliwa”alisema Kanyasu.

Kanyasu ameliambia Tanzania Daima kuwa katika awamu ya pili atatoa kipaumbele kwa wakazi wa Mtaa wa Moringe kuwachongea barabara nzuri ili kuharakisha maendeleo yao.

MWISHO



Thursday, September 7, 2017

Mfanyabiashara Atuhumiwa kwa uchafuzi wa Mazingira




Na antony Sollo Geita
07.09.2017

MFANYABIASHARA Ernest Nyororo mkazi wa Geita analalamikiwa na wananchi kwa uchafuzi wa Mazingira ikiwemo kuathiri Afya za wananchi  kutokana na kusimika mashine za kusaga na kukoboa mpunga katika maeneo ya makazi  ya watu na kusababisha mvutano na viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Moringe Tanzania Daima limeelezwa.


Akizungumza na Tanzania Daima Mwenyekiti wa Mtaa wa Moringe Adriano Rwechungura alisema kuwa Ofisi yake imejitahidi kusuluhisha jambo hili kwa kuiandikia barua Ofisi ya Mkurugenzi wa Mtendaji wa Mji wa Geita bila mafanikio ambapo hata hivyo walichukua hatua ya kumuandikia Mratbu wa NEMC Kanda ya Ziwa kwa hatua zaidi kwa madai kwamba Nyororo anatumia fedha zake kama fimbo ya kuwanyanyasa wananchi wanyonge.


“Sisi tumechukua hatua ya kumuandikia Mratibu wa NEMC Kanda ya Ziwa kutokana na jeuri ya mwekezaji huyu maana anatumia fedha zake vibaya kwamba tumeandika barua zaidi ya mara tano lakini hatuoni mabadiliko yoyote ambapo tumeona kila maafisa wanapoenda pale wananyamazishwa kwa fedha hatimaye tukachukua hatua hii”alisema Rwechungura

Tanzania Daima limepata nakala ya barua ya malalamiko yenye kumb Na NEMC/MZA/CMP/VOL1/49 iliyoandikwa na Mratibu wa baraza la Mazingira Kanda ya Ziwa kwenda kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Geita ya tarehe 13/12/2016 ikikiri kupokea barua ya malalamiko kuhusu kero ya vumbi inayotokana na Mashine za kusaga na kukoboa mali ya Ernest Nyororo makazi wa Geita.

Katika barua hiyo,Mratibu wa NEMC Kanda ya Ziwa Jamal Baruti anamuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Geita kushughulikia kisheria suala hilo kwa kutumia kanuni na taratibu za Mazingira Mipango miji na Afya.

“Tunaomba suala hili lishughulikiwe kulingana na Sheria kanuni na taratibu za Mazingira Mipango miji na Afya kwani tunaamini kwamba utatuzi wa jambo hili ko ndani ya mamlaka ya Halmashauri”ilisema sehemu ya barua hiyo.

Kwa mujibu wa Kanuni na taratibu za Mazingira Maafisa wa Mazingira wa Wilaya na Miji wanayo mamlaka kamili ya kuhakikisha Sheria ya Mazingira ya 2004 inasimamiwa na kutekelezwa ipasavyo,aidha Maafisa wanaosimamia mipango miji na masuala ya Afya wanayo pia mamlaka ya kuhakikisha Sheria husika zinasimamiwa na kutekelezwa.

Hata hivyo Gazeti hili lilimtafuta Ernest Nyororo kuzungumzia mgogoro huo ambapo alikana na kusema kuna msuguano mkali dhidi yake na mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Moringe  Adriano Rwechungura ambaye Nyororo alidai kuwa Mwenyekiti huyo anatumia njia za kifisadi kutaka kumchafua.
“mimi sijakaidi maelekezo ya baraza la Mazingira isipokuwa kuna tatizo kubwa la kutokuwepo kwa maelewano na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Adriano Rwechungura amejificha nyuma ya jirani yangu ambaye hata hivyo nilipopewa maelekezo na watu wa NEMC kuziba mabati hapo kwenye eneo langu ndivyo nilivyofanya je walitaka nifanye nini zaidi?alihoji Nyororo.

Kwa upande wake Afisa wa Mazingira wa Halmashauri ya Mji wa Geita aliyefamika kwa jina moja la Shwekelela alipotafutwa kuzungumzia sakata hilo alisema yuko nje na Ofisi hivyo kuahidi atafutwe siku nyingine ambapo Tanzania Daima lilimtafuta tena kupitia namba ya mkononi 0785 909 308 ambapo simu hiyo iliita bila majibu na juhudi za kumtafuta zinaendelea.

MWISHO



Sunday, July 16, 2017

Barua ya Wazi kwa Waziri wa Fedha.





Mh Waziri,
Naomba kuwasilisha Malalamiko yangu kwako kuhusu vitendo nilivyofanyiwa na
kampuni ya Tujijenge Microfinance iliyoko katika mtaa wa New Bagamoyo Rd. Plot 17, Block 45A yenye Makao yake Makuu jijini Dar es salaam Dar Es salaam

 Mimi ni mwananchi mkazi wa jiji la Dar es salaam, niliomba Mkopo wa Shilingi milioni arobaini (40,000,000/) kwa ajili ya kuimarisha biashara yangu tangu 25 March mwaka huu na kutimiza masharti ikiwemo kufanyiwa tathmini ya biashara yangu  hivyo kukubaliwa kupatiwa fedha nilizoomba lakini hadi sasa niko njiapanda sijui la kufanya japokuwa kwa mujibu wa mashharti ya Kampuni hiyo  nilitakiwa niwe nimepatiwa mkopo huo ndani ya siku saba baada ya kukamilisha masharti ya mkopo huo.

Mh Waziri nimesikitishwa na watendaji wa Shirika hilo baada ya kuniingiza katika mgogoro mkubwa kutokana na kuchukua mkopo katika taasisi  ndogo za fedha baada ya kuhakikishiwa kuwa nimefuzu kupatiwa mkopo huo ndani ya siku saba lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea.

Nilikuwa na mpango wa kukuza biashara yangu kwa kununua basi kwa ajili ya kusafirisha wanafunzi ,nimesumbuliwa sana,nimetumia zaidi ya shilingi milioni mbili kwa ajili ya mawasiliano usafiri paomja na muda na kuingia madeni yaliyopelekea kuchukuliwa vitu vyangu nilivyoweka kama dhamana .kutokana na ahadi niliyokuwa nimetoa kwa wateja wangu kwamba ningekamilisha suala hilo kwa muda lakini hadi sasa  sijui kinachoendelea.

Kufuatia hali hii nimeingia gharama kubwa  yakiwemo madeni kutokana na ahadi za watendaji wa Kampuni hii zinazofikia mil 2 pamoja na kuchukuliwa kwa mali zangu zenye thamani zaidi ya shilingi milioni nane ambapo jumla ya madai yote ni shilingi milioni kumi( 10,000,000 ) na ninaomba uingilie kati mgogoro huu kufuatia baadhi ya  taasisisi za fedha kuendesha shughuli zao bila kuzingatia Sheria za Nchi.
Nimejitahidi kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huu bila mafanikio sasa naomba msaada maana mpaka sasa nimeingia katika matatizo makubwa ikiwemo kuyumba kwa uchumi na mahitaji ya familia maana nimetumia fedha nyingi katika ufuatiliaji ikiwemo kuweka mafuta kwenye magari ya maafisa wa Shirika hilo kwa nyakati tofauti hasa baada ya kuhakikishiwa kuwa nimefuzu kupata mkopo lakini hadi sasa nimetelekezwa.

Kwa barua hii naiomba Serikali iingilie kati suala hili ili haki iweze kutendeka.

BARAKA BEATUS MASHAURI
                                       S L P
                                       DAR ES SALAAM

Monday, February 27, 2017

Wanafunzi Buhongwa B wasomea chini ya mti.




Na Antony Sollo Mwanza

WANAFUNZI wa Shule ya Msingi Buhongwa B iliyoko katika Jimbo la Nyamagana Mkoani Mwanza wanasoma wakiwa chini ya mti wakiwa hawana hata Madawati ya kukalia kufuatia changamoto kubwa za Vyumba vya Madarasa Matundu ya vyoo na nyumba za walimu zinazoikabili shule hiyo Tanzania Daima limebaini.

Mwandishi wa Tanzania Daima aliyefika shuleni hapo alishuhudia wanafunzi zaidi ya mia moja wakisomea nje chini ya miti huku kukiwa na wingu zito la mvua  ambapo baada ya kufuatilia kwa wahusika kujua tatizo ni nini walimu wa shule waligoma kueleza chochote na kumuomba Mwandishi huyo akaonane na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Kiomoni Kibamba kwa kuwa yeye ndiye msemaji mkuu.

Mwandishi wa gazeti hili alimtafuta Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza kuzungumzia suala hilo ambapo alikiri kuwepo kwa upungufu mkubwa wa vyumba vya Madarasa.

“Tuna changamoto kubwa ya vyumba vya Madarasa hii inatokana na idadi kubwa ya wanafunzi ambapo kwa mwaka 2016 tuliandikisha wanafunzi 500 na mwaka 2017 hadi jana 27 feb tumeandikisha wanafunzi 450 jumla ya wanafunzi wote kwa sasa ni 950 katika Shule hiyo”alisema Kibamba.

Akifafanua Mikakati waliyo nayo Mkurugenzi huyo alisema kuwa Mwaka 2016 waliandikisha wanafunzi  8000 katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana na mwaka 2017 kuna wanafunzi zaidi ya 8000 ambapo mpango wa Elimu bure ulitangazwa na Rais Magufuli umesababisha ongezeko kubwa la wanafunzi na kuvuka malengokatika uandikishaji wa wanafunzi.

Hadi Sasa Serikali imepeleka Shilingi mil 15,000,000 katika Shule hiyo kwa ajiri ya ujenzi wa vyumba vya madarasa huku Shilingi Mil 900,000,000 zikipelekwa Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana ajiri ya kukamilisha mradi wa madawati ya akiba ili kukabiliana na ongezeko lolote litakalojitokeza baada ya kukamilika kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa shuleni hapo

Kwa upende wake Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Stanslaus Mabula alikiri kuwepo kwa changamoto zinazoikabili shule hiyo ambapo Mabula alisema kuwa ni kweli kuna upungufu mkubwa wa vyumba vya Madarasa, Nyumba za walimu, matundu ya vyoo pamoja na majengo ya Ofisi za Walimu.

“Tuna uhaba mkubwa wa vyumba vya madarasa katika jimbo letu la Nyamagana lakini pamoja na hayo tumejitahidi kwa upande wa Madawati tumefanikiwa kukamilisha idadi inayotakiwa na hadi sasa tuna ziada ya madawati 3000 yakiwa hayana pa kuyaweka.

Akizungumzia mikakati waliyonayo kukabiliana na changamoto hizo Mbunge huyo alisema kuwa wanahamasisha wadau mbalimbali ikiwemo Serikali kuu pamoja na wananchi katika maeneo mbalimbali jimboni humo kuchangia ujenzi wa vyumba vya Madarasa vipatavyo 24 ili kuweza kuanzisha Shule mpya kupunguza mrundikano wa wanafunzi katika shule mbalimbali jimboni humo.

“Tuna upungufu wa vyumba vya Madarasa vipatavyo 1200 na hadi sasa tunaendelea kuhamasisha wadau mbalimbali kuchangia ujenzi wa vyumba vya Madarasa vipatavyo 24 kwa ajiri ya kuanzisha Shule mpya ili kupunguza mrundikano wa wanafunzi katika shule mbalimbali katika jimbo letu”.alisema Mabula.

MWISHO