Ajichinja kwa wivu wa Mapenzi
Na Antony Sollo Mpwapwa.
Mtu mmoja amenusurika kifo katika
stendi ya mabasi Wilayani Mpwapwa baada ya kujichinja kwa kutumia kitu chenye
ncha kali kwa kile kilichodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Tukio hilo limetokea Oktoba 25
majira ya saa 7: 53 mchana katika stendi ya mabasi Wilayani Mpwapwa, mtu huyo
ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja alichukua uamzi huo baada ya
kukataliwa na mwanamke aliyedaiwa kuwa alikuwa ni mpenzi wake.
Chanzo cha taarifa kutoka Wilayani
Mpwapwa zimeeleza kuwa kijana huyo ni mgeni katika maeneo hayo na kwamba
alikuja kumfuatilia mpenzi wake akitokea Mkoani Iringa ambapo baada ya kufika
katika maeneo hayo,alikuta mpenzi wake akiwa na mwanamme mwingine jambo lililosababisha
kuchukua uamzi wa kujitoa roho
Hata hivyo juhudi za kujitoa uhai
kwa kijana huyo ziligonga mwamba baada ya Askari wa Jeshi la Polisi kufika
katika eneo la tukio kumchukua na kumkimbiza
hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa kwa matibabu.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani
Dodoma alipotafutwa kwa simu yake ya mkononi kuzungumzia tukio hilo simu yake
iliita bila majibu na juhudi za kumtafuta zinaendelea ili kuweza kuthibitisha
taarifa hizo