Saturday, September 9, 2017

Wananchi Maganzo waiponda Kamati ya Ndugai.



·        Wasema iliacha kuangalia matatizo ya wananchi
·        Ilienda kwa ajili ya kuangalia madini pekee.
·        Wasema huo si uzalendo,Utaifa.
·        Kamati hiyo haikufanyi kazi Mgodi wa Elhilal ulioko hapo

Na Antony Sollo Shinyanga.
09.09.2017

WANANCHI wa Mji mdogo wa Maganzo Wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga wametoa maoni yao kuhusu ripoti iliyowasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli huku wakiiponda Kamati iliyoundwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai wakisema Kamati hiyo ina mapungufu makubwa Tanzania Daima limeelezwa.

Akizungumza na gazeti hili mmoja wa wahanga wa mgodi huo George Joseph ambaye alipigwa risasi na walinzi wa mgodi huo ameilalamikia Kamati hiyo kwa kushindwa kuangalia maisha ya Raia na badala yake Kamati hiyo imedaiwa kujikita zaidi kuangalia wizi wa Madini ya Almasi katika Mgodi mmoja huku Mgodi unaomilikiwa na Phantom ambaye anamiliki Kampuni ijulikanayo kama Elhilal Mining ukiachwa bila kuchukuliwa taarifa zake yakiwemo mauaji ya wananchi wakazi wa Maganzo.

“ Ripoti ya Kamati hii ina mapungufu makubwa sana kwani ujio wake haukulenga kukutana na wahanga na pia ilipata makengeza kwa kushindwa kuuona mgodi wa Elhilal Mining unomilikiwa na Pantom ambapo Kamati hiyo imekutana na watu ambao taarifa zao zimejikita kwenye madini pekee lakini haikukumbuka kama kuna matukio makubwa ya Mauaji, unyanyasaji wa raia kama ilivyokuwa katika Kamati iliyoundwa kuchunguza zoezi la Operation Tokomeza ambapo Kamati hiyo ilizama zaidi katika masuala ya Haki za Binadamu kujua matatizo yiyowapata raia”alisema George.

George ameeleza kusikitishwa kwake na ubaguzi uliofanywa na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Nyabaganga Talaba kwa kuwazuia waathirika waliopigwa risasi na walinzi wa Mgodi wa Mwadui kuingia katika kikao cha Kamati hiyo ili kueleza hali halisi na yanayojili kila siku katika Mgodi wa Mwadui na kwamba eneo la Mgodi wa Mwadui halimilikiwi na WDL pekee bali kuna mwekezaji mwingine ambaye amekuwa tishio kwa usalama wa raia kutokana na kuua vijana wengi na haku akilindwa na viongozi wa Serikali na hadi sasa hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi yake.

“Mwekezaji huyu ameua watu wengi na viongozi wa Jeshi la Polisi na Madaktari waliokuwepo kipindi cha awamu ya Nne walikuwa na mnyororo mkubwa wa rushwa ambapo vijana wengi waliuawa na kupelekwa gerezani huku mmiliki wa Kampuni ya Elhilal akishinikiza vijana wanaokamatwa kupelekwa gerezani na kuwekwa mahabusu kwa lengo la kutukomoa,Phantom amediliki kunyang’anya maeneo ya watu lakini Serikali ilikuwa imewekwa mfukoni hebu tumuombe Mh Rais aje tumweleze mateso tuliyo nayo sisi wananchi wa Maganzo”alisema George.

Kwa mujibu wa George Joseph ambaye ni mmoja wa waathirika kutokana na kupigwa risasi na walinzi wa mgodi wa Mwadui  ni kwamba kuna makundi mbalimbali yaliyoachwa kusikilizwa na Kamati ya Ndugai na bila kuyataja makundi hayo ripoti hiyo inakuwa haijakamilika na inakuwa na doa lisilofutika.

Uchunguzi uliofanywa na Mwandishi wa gazeti hili umebaini kuwa Kamati hiyo ilipata kigugumizi cha kukutana na wahanga waliopata ulemavu kutokana na kushambuliwa kwa risasi za moto na walinzi wa Kampuni ya Zenity Security inayolinda rasrimali za mgodi wa Mwadui pamoja na walinzi wa Kampuni ya Elhilal Mining ambapo baada ya kulalamika sana wahanga hao waliahidiwa na Kamati hiyo kwamba wangekutana na Wajumbe wa Kamati hiyo Mjini Dodoma kabla ya kukabidhi Ripoti kwa Rais John Pombe Magufuli na sasa wanajiuliza! kwa kuwa Kamati hiyo imekabidhi ripoti hiyo bila kuwasikiliza watapata wapi tena nafasi ya kukutana ili waweze kueleza matatizo yao?


Katika hatua nyingine George na wenzake wamemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya uchunguzi wa Viongozi wa Jeshi la Polisi waliokaa muda mrefu Mkoani Shinyanga maana kuna taarifa za kuwepo kwa namna Fulani ya ushirikiano kati ya taasisi za Serikali na Makampuni yanayofanya shughuli zake katika eneo la Mwadui.

“ kuna kesi nyingi za mauaji,kujeruhi kwa silaha za moto zimekuwa zikizimwa muda mrefu kwa ushirikiano wa madaktari wa Hospitali ya Serikali wakati wa uchunguzi wa majeruhi zikiwemo maiti baada ya mauaji yanayotokana na walinzi wa mgodi wa Mwadui na Elhilal inayomilikiwa na Phantom”.alisema George.

Ameyataja makundi hayo kama ifuatavyo.

Waliopigwa risasi na kupata ulemavu wa kudumu.

Katika kundi hili George anasema liko na watu wafuatao, yeye mwenyewe George Joseph Bwisige (alipigwa risasi na kupelekea kukatwa mguu wa kulia lakini hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa),Hamud Said , Marco Ngussa (ambaye alipigwa risasi na kupasuliwa bandama),Nyalulu Sitta (alipigwa risasi na kutobolewa jicho),

Kundi lingine ni la watu waliouawa kwa kupigwa risasi na Askari wa mgodi.

Hawa ni Benard Edward maarufu (Mayo), Shilagi Masali mkazi wa Masagala,Jishosha Daud, Hamad Shunda Mkazi wa Ikonongo ambaye hakuonekana isipokuwa nguo zake pekee tu ndiyo zilizoonekana

Hawa ni kundi dogo tu ambao taarifa zao zimeweza kupatikana na wengi wamepotelea katika mashimo yenye kina kirefu baad ya kukimbizwa wakielekezwa huko kwa lengo la kuwaua na wanamuomba Rais Magufuli aweze kuangalia utaratibu unaofaa ili kuwapatia kifut jasho waweze kukidhi mahitaji ya kibinadamu maana wamefanyiwa ukatili usiowezakusahaulika maishani mwao.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekabidhiwa Ripoti Maalumu ya kuchunguza Biashara ya Madini ya Almasi na Tanzanite nchini 7 Agosti 2017 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa tukio lililofanyika katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam.

Kabla ya kukabidhiwa Ripoti hizo  kwa Rais Magufuli na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai alizipokea ripoti hizo kutoka kwa Wenyeviti wa Kamati Maalumu alizoziunda ambazo zilijumuisha Wabunge wa Bunge la Tanzania kutoka vyama mbalimbali vya Siasa.

Kamati hizo ziliongozwa na Dotto Biteko aliyeongoza Kamati ya kuchunguza biashara ya Madini ya Tanzanite na Mussa Azzan Zungu Kamati ya kuchunguza biashara za Madini ya Almas.

 Kamati hizo ziliundwa wakati wa Mkutano wa Saba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kuchunguza mfumo bora wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa biashara ya madini ya Almas na Tanzanite.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa ripoti hizo, Rais Magufuli amemtaka Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwaita Wataalamu na Taasisi zote zinazohusika na masuala ya madini kufanya maandalizi ya kubadili Sheria zitakazosaidia Taifa kunufaika na rasilimali zake za madini.

 “ Huu ndiyo wakati wa kubadilisha sheria zetu. Mhe, Waziri Mkuu uwaite Wataalam wote wanaohusika na madini maandalizi haya yaanze haraka,” amesema Dkt. Magufuli.

Aidha, Rais Magufuli amesisitiza suala la uzalendo kwa Watanzania wote katika kusimamia rasilimali za nchi na kusema kuwa, ikiwa watanzania wataweka mbele uzalendo Taifa litasimama na kwamba hatutochezewa na wawekezaji tena na mikataba mibovu ambayo italiingizia Taif letu hasara.

Dkt. Magufuli amesema hivi sasa uchumi wa Tanzania unakua kwa asilimia 7 hadi 7.1 na nchi ya nne nyuma ya nchi ya Ethiopia ambayo uchumi wake unakua kwa asilimia 8.3 na kueleza kuwa, iwapo rasilimali hizo zingesimamiwa vizuri taifa lingenufaika zaidi na kuwa na uchumi zaidi ya nchi ya India ambayo haizalishi madini ya Tanzanite lakini imekuwa ni muuzaji mkubwa wa madini hayo.

 “ Tutangulize maslahi ya nchi yetu mbele,nataka tufike mahali tuanze upya,Mhe. Spika muendelee kutusaidia katika kusimamia rasilimali zetu, amesema Dkt. Magufuli.”

Katika hatua nyingine Rais Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Wateule waliotajwa katika ripoti hiyo kukaa pembeni ili kupisha vyombo vya Ulinzi na Usalama kufanya kazi yake vizuri.

Rais Magufuli amesema hayo yote yanafanyika ili kuh akikisha kwamba watanzania wananufaika na rasilimali hizo na kueleza kuwa, bado watanzania hawajanuifa vya kutosha na rasilimali za nchi ikilinganishwa na rasilimali zilizopo.

Awali, akizungumza wakati wa kukabidhi Ripoti hizo, Waziri Mkuu Majaliwa alisema kuwa, Kamati mbili zilizoundwa na Spika wa Bunge zimefanya kazi kubwa na hali hiyo inatokana nia ya dhati aliyoionyesha Rais Magufuli kuhakikisha,rasilimali za madini zinakuwa na tija kwa Taifa.

 Kwa upande wake Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai alisema kuwa, Bunge liko tayari kuzipitia na kuzifanyia marekebisho Sheria zote ambazo hazilinufaishi Taifa na kueleza kuwa ipo haja ya kulifanyia kazi suala la mifumo ya udhibiti wa rasilimali hizo.

Ndugai amewataka viongozi wa Serikali waliopewa dhamana ya kusimamia shughuli za Umma kuguswa na umaskini wa Watanzania na hivyo kuzitaka Bodi mbalimbali nchini kubadilika na kuona haja ya kuangalia na kufuatilia kwa karibu maeneo wanayoyasimamia.

Akiwasilisha ripoti ya Madini ya Almasi Mwenyekiti wa Kamati hiyo  Mussa Azzan Zungu alisema soko la madini ya Almasi bado liko katika kiwango duni japokuwa Almas yenye thamani ya juu inapatikana Tanzania pekee.
a
 Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Tanzanite Dotto Biteko alieleza kuwa, asilimia 80 ya Tanzanite inatoroshwa nchini na asilimia 20 ya madini hayo ndiyo yanayoingia katika mfumo wa kodi nchini.


MWISHO.