Saturday, January 20, 2018

Serikali Yapiga Marufuku Kulima Pamba kwa Mkataba



Zao la Pamba likiwa Shambani picha na Maktaba.
WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali imekataza kilimo cha pamba cha mkataba kwa sababu kinawanyonya wakulima.
Waziri Mkuu ameyasema hayo jana (Ijumaa, Januari 19, 2018) wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua zahanati ya Hunyari wilayani Bunda, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mara.
“Ni marufuku kwa wanunuzi wa pamba kulima pamoja na wakulima kwa sababu wakulima wanakosa uamuzi wa kupanga bei. Kuanzia sasa zao hilo litauzwa kwa njia ya mnada.”
Alisema Serikali imeweka mkakati wa kuimarisha mazao makuu ya biashara ambayo uzalishaji wake umeanza kupungua likiwemo na zao la pamba.
Waziri Mkuu alisema Serikali imeamua kushiriki kikamilifu katika usimamizi wa kilimo cha zao la pamba kuanzia hatua za maandalizi ya shamba, pembejeo hadi masoko.
Pia Waziri Mkuu amewaagiza Maofisa Kilimo katika wilaya hiyo wawafuate wakulima vijijini kwa ajili ya kutoa elimu itakayowawezesha wakulima kulima kwa kufuata njia bora za kisasa.Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wafugaji kuhakikisha wanakuwa na idadi ya mifugo kulingana na uwezo wa eneo lao.“Marufuku kulisha mifugo katika mashamba ya watu.”
Amesema Serikali itachukua hatua kali za kisheria kwa mfugaji yeyote atakayelisha mifugo yake katika mashamba ya wakulima kwani tabia hiyo huchangia migogo baina yao.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
Source: MCHAMBUZI BLOG / 16 minutes ago