Sunday, February 11, 2018

Afisa biashara Manispaa ya Ubungo awaliza mamilioni wafanyabiashara .

Na  Antony  Sollo Ubungo.

AFISA biashara wa Manispaa hiyo Geofry Mbwama anatuhumiwa kujipatia mamilioni ya fedha toka kwa wafanyabiashara wenye maduka pamoja na wajasiriamali katika manispaa hiyo baada ya kuingia kila duka akiomba Leseni ya biashara akiwa na Dereva wa Manispaa hiyo na kufanikiwa kujipatia kiasi kikubwa cha fedha akitumia nyaraka bandia za Serikali Tanzania Daima libaini.

Tukio hilo lilitokea desemba 13 mwaka jana katika Mtaa wa Mbezi Luis Manispaa ya Ubungo Jijini Dar Es Salaam ambapo Mbwama akiwa na gari la Manispa hiyo aliingia katika maduka na vibanda vya wafanyabiashara wadogo mafundi pikipiki hata wanaofanyia shughuli zao nje huku akihoji kama wana Leseni za biashara na pale ambapo alikuta hawana kwa sababu mbalimbali alifunga biashara na makufuli yake na baadaye aliandika nyaraka inayodaiwa kuwa ni feki na kuwapiga faini kati ya 321,000.

Akithibitisha kufanyiwa vitendo hivyo mmoja wa wajasiriamali (Fundi pikipiki) eneo la Mbezi makabe road Rahesh Shaban ambaye anajishughulisha na ufundi wa pikipiki alisema alilazimishwa kufunga shughuli zake baada ya kubainika kuwa hakuwa na leseni ya kufanya kazi ya ufundi licha  ya kujitetea kuwa alikuwa ameenda katika mamlaka ya Mapato Tanzania kwa ajili ya kupatiwa namba ya utambulisho wa mlipa Kodi ( TIN Number) lakini Afisabiashara huyo alimwandikia faini ya shilingi 321,000 na kumwamuru afunge shughuli zake.

“Mimi na wenzangu hapa tumemweleza kuwa tunazo baadhi ya nyaraka na kwamba tayari tulikuwa tumeshaanza mchakato wa kupatiwa namba ya utambulisho ya mlipa kodi( TIN Number) lakini hakutuelewa na matokeo yake aliandika faini katika nyaraka ambazo tunahisi ni feki kwa kuwa nyaraka yoyote ya Serikali huwa haiandikwi kitu chochote au namba ya mtu binafsi ambapo hata hivyo aliomba fedha kiasi kati ya 20,000, mpaka 60,000 tukampatia na hakutoa risiti yoyote”alisema Shabani.

Kwa kuwa Shaban aliona kuwa mahala pale ndipo anapopata riziki kwa ajili ya mahitaji ya familia yake,aliomba asamehewe lakini kilichoshangaza aliombwa shilingi 20,000 na Mbwama lakini hakupatiwa risiti jambo ambalo pia lilithibitishwa na wafanyabiashara wa duka la madawa yaliyoko jirani na Shabani ambao nao walitoa fedha kiasi cha shilingi 60,000 kila mmoja kutokana na kutishiwa kufungiwa maduka yao ambapo fedha hizo zilikabidhiwa kwa dereva wa Manispaa ambaye naye alikuwa akiwakaripia wafanyabiashara na kutoa vitisho vya kuwafungia biashara zao.

Tanzania Daima lilifuatilia nyendo za Mbwama na kukutana na malalamiko lukuki kwamba wafanyabiashara na wajasiriamali wa Mtaa wa Mbezi walio wengi walikuwa wameshachukuliwa fedha zao kutokana na tishio la kufungiwa biashara zao na Afisa biashara huyo akishirikiana na dereva wake.

Mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima alimtafuta Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo ambapo hata hivyo juhudi za kumpata Mkurugenzi huyo ziligonga mwamba kutokana na mwingiliano wa majukumu ambapo lilikutana na Katibu Tawala James Mkumbo ambaye baada ya kupatiwa taarifa juu ya kilichofanywa na watumishi hao dhidi ya wafanyabiashara nawajasiriamali na kuahidi kuzifanyia kazi tuhuma hizo ambapo tangu 13 desemba hadi leo hakuna taarifa zozote.

Mara kadhaa Mkumbo amekuwa akitakiwa kutolea ufafanuzi wa tatizo hilo lakini amekuwa akidai kuwa alikabidhi watu kufanyia kazi tuhuma hizo
“Kwa sasa niko Mwanza lakini kuna watu niliwapa jukumu la kushughulikia suala hilo lakini pia sisi hatufanyi kazi kwa pressure za waandishi wa Habari kwa sababu wanataka habari tukikamilisha utaratibu wetu tutafanya kinachostahili ”alijibu  Mkumbo kwa njia ya ujumbe wa simu ya mkononi.

Kinachoshangaza hapa ni kwamba hakuna taarifa zozote kuhusu ufuatiliaji wa tuhuma hizi pamoja na Katibu Tawala huyo kupelekewa Ofisini tuhuma zinazowakabili Afisa biashara wa Manispaa pamoja na dereva wa Manispaa ya Ubungo kwa takribani miezi miwili sasa jambo linalozua sintofahamu juu ya uadilifu wa watumishi hao

Wananchi waliozungumza na gazeti hili wameiomba Serikali kuwachunguza baadhi ya wafanyakazi wake hasa waliotumbuliwa kwa kuwa sasa wengi wako mtaani hawana kazi na wamegeuka Matapeli wanaotumia mbinu walizokuwa wamezizoea wakiwa kazini kutafuta fedha kwa njia za vitisho na inasemekana Mbwama na dereva wa Manispaa ya Ubungo kwa pamoja wamejipatia mamilioni kwa njia hiyo.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo John Kayombo hakuwez kupatikana mara moja kuzungumzia tuhuma hizo ambapo juhudi za kumtafuta atolee ufafanuzi wa hatua gani zimechukuliwa dhidi ya tuhuma kwa watumishi hao kwa kukiuka maadili ya Utumishi wa Umma

MWISHO.