Na Antony Sollo
Februari 9,2018.
WANAUME katika halmashauri ya mji wa Kahama
Mkoani Shinyanga wametakiwa kuachana na dhana ya kujimilikisha hati
miliki za viwanja vyao, ili kutoa kipaumbele kwa akinamama ili nao
waweze kumiliki ardhi hali ambayo itaepusha migogoro katika
familia.
Akizungumza kabla ya kutambulisha mradi wa upimaji wa
viwanja 4,000 katika kata ya Mhongolo afisa ardhi wa halmashauri ya
mji wa Kahama Mashiri Magasa alisema kuwa wanaume
wilayani Kahama wamekuwa na tabia ya kujimilikisha maeneo yote yenye hati
miliki jambo ambalo siyo haki na kwamba hali kama hiyo pindi mwanaume
anapofariki dunia humwacha mwanamke katika wakati mgumu.
Magasa aliyasema hayo februari 8 mwaka huu wakati
akizungumza na wananchi wa vitongoji vya sofi, bomani na Nyamhela vilivyoko katika
Mtaa wa Mhongolo ambapo aliwaasa wanaume kuachana na dhana ya kujimilikisha
maeneo ya familia kwani hali hiyo ndiyo chanzo cha mifarakano katika familia
pindi baba wa familia anapoamua kuchukua hati hizo na kuomba mkopo katika
taasisi za fedha na kushindwa kurejesha.
“Ifike wakati wanaume muwape fursa ya kumiliki ardhi wanawake
kwani kufanya hivyo kunatoa usawa katika familia lakini pia kuna wakati mmoja
wa familia hiyo akifariki hasa baba mwanamke hawezi kuhangaika kutokana kuwa
tayari anakuwa ana mali halisi inayomfanya aendeleze familia, wanaume wakiachana
na mfumo dume mwanamke akashirikishwa ipasavyo katika umiliki huo
hakutakuwepo na migogoro baina yao,” Alisema Magasa.
Katika hatua nyingine Afisa ardhi aliwataka wakazi wa
mji wa Kahama kuhakikisha wanapima viwanja vyao kabla ya kufanya ujenzi au
shughuli zozote za kimaendeleo na upimaji huo uende sambamba na utafutaji wa
hati miliki ili kupunguza migogoro isiyokuwa na tija kwa jamii na kuwafanya
waweze kukopesheka kirahisi katika taasisi za fedha.
“Kwa mujibu wa sheria ya Ardhi na mpango miji hakuna
mwananchi yoyote hapa nchini anayeruhusiwa kufanya ujenzi wowote wa nyumba za
makazi katika kiwanja chake bila ya kupimwa au kujenga nyumba bila ya kufuata
ramani za mpango miji tukikuta unajenga kwenye eneo bila kibali tunasitisha
ujenzi na kukupiga faini” alisema Magasa.
Kwa mujibu wa mpima ardhi kutoka kampuni
ya Total Geo survey Co.Ltd
Emmanuel William ambaye anayeshughulikia upimaji wa
viwanja katika kata hiyo alisema kuwa wananchi wanatakiwa
kuchangia gharama za upimaji ili kazi iweze kuendelea na kwamba
mpaka sasa viwanja 4,000 vimepimwa na viwanja 1000 vimepitishwa
na wizara ya ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa
ajili ya kuwatafutia hati miliki wananchi.
Akizungumzia zoezi hilo William alisema kuwa lengo ni
kupima viwanja 12,000 katika Kata hiyo na kuwataka wananchi kuongeza kasi ya
kuchangia gharama ya upimaji ambayo ni shilingi elfu tisini 90,000 na kwamba
gharama hiyo ni ndogo ukilinganisha na bei elekezi ya serikali ya kuanzia ambayo
inaanzia shilingi laki tatu, 3,000,000. Kwa kila kiwanja.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa mtaa wa Mhongolo
Denis Diocles alisema kuwa lengo la kampuni hiyo ni kupima
viwanja elfu 12, lakini viwanja vilivyofikiwa ni 4021, vilivyopewa namba ni
1335, ambavyo havijapewa namba ni 2686 na kutaja mradi wote unagharimu kiasi
cha shilingi milioni 361 kati ya hivyo vilivyolipiwa ni 1192 na ambavyo
havijalipiwa ni 2828.
Akizungumza katika zoezi la kutamburisha mradi huo Mwenyekiti
wa mtaa wa Mhongolo Emmanuel Nangale alisema kuwa kukusanya shilingi milioni
361 kwa wakazi hao siyo kazi ndogo na kudai kuwa kiasi kilichokusanywa
hadi sasa kinapswa kupongezwa licha ya watu kutohamasika kikamilifu na kwamba
katika halmashauri hiyo ni Mtaa wa Mhongolo pekee umejitutumua katika zoezi
hilo.
Mwisho.