Monday, February 19, 2018

Hongera Waziri Mkuu kufanya ziara Mwanza

Antony Sollo  Misungwi

Ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Jijini Mwanza imekuwa ya mafanikio,hii ni baada ya kubaini mambo uozo lakini haya ni kwa uchache kutokana na siri kubwa iliyofichika kutokana uozo mwingi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza.

Historia ya kuwepo kwa Uozo Misungwi.

Wilaya ya Misungwi ni moja kati ya Wilaya kongwe nchini ambazo zimekuwa zikiongoza kwa kupata hati chafu na imekuwa bahati kwa Mawaziri Wakuu wa awamu ya Nne na ya tano ambao wote wamebahatika kukumbana na uozo jambo lililopelekea kuwatumbua watumishi wachache wa Halmashauri hiyo huku vinara wakiachwa kutokana na kuwepo kwa mnyororo mkubwa ambao umetengenezwa maalumu kwa ajili ya upigaji dili.

Katika ziara yake hivi karibuni,Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Khassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi,  Alphonce Sebukoto,  na kuagiza achungunzwe na vyombo husika.

Waziri Mkuu alifikia hatua hiyo baada Mwanasheria huyo kuonekana kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kushindwa kuishauri vyema halmashauri hiyo na kuisababishia hasara ya sh. milioni 279.


Majaliwa alimsimamisha kazi Sebukoto 19februari mwaka huu wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa halmashauri hiyo akiwa katika ziara ya siku tano ya kikazi mkoani Mwanza ambapo waziri Mkuu alisema.

“Mwanasheria utasimama kazi kuanzia leo na tuhuma zako zitachunguzwa kikamilifu na vyombo husika na uchunguzi ukibaini kama huna kosa utarudi kazini. hatutakuonea lakini hatuwezi kukuvumilia kwa utaratibu huo ulioufanya,” alisema Majaliwa.

Imeelezwa kuwa Novemba 2017 wakati alipokuwa anakaimu nafasi ya Ukurugenzi Mwanasheria huyo aliidhinisha malipo ya sh. milioni 279 zilipwe katika akaunti binafsi ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Antony Bahebe.

Kwa mujibu wa taarifa ya Waziri Mkuu Bahebe aliishtaki halmashauri hiyo akidai kulipwa fedha kwa ajili ya kazi ya ukandarasi wa mradi wa maji Igenge uliojengwa na kampuni ya ukandarasi ya Seekevim ambapo alisema  mradi huo ulianza 2014 na ulitakiwa ukamilike 2015,ambapo  Mwanasheria huyo aliidhinisha malipo hayo wakati ambao tayari hati maalumu ya uwakilishi ilikuwa imekwisha tangu Desemba 2015.

“Mwanasheria amemlipa Mwenyekiti wa Halmashauri kwa kufanya kazi na Halmashauri baada ya kuifikisha Halmashauri yake Mahakamani. Amemlipa fedha wakati kazi yenyewe ilikuwa haijaisha na aliharakisha malipo hayo kipindi ambacho Mkurugenzi hayupo, ”alisema Majaliwa huku  akiwakumbusha watumishi wa umma kuzingatia maadili ya utumishi na matakwa ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akifafanua Majaliwa alisema fedha alizolipwa Bahebe zingeweza kutumika katika ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri hiyo.

Katika ziara hiyo Waziri Mkuu alifungua mabweni ya watoto wenye mahitaji maalumu katika shule ya msingi ya Mitindo iliyoko wilayani Misungwi na pamoja na kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Ukiacha na kipande hicho cha uozo uliofichwa,Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi imekuwa na historia mbaya kwa watendaji wa Wilaya hiyo kutafuna fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo baadhi ya watendaji wa halmashauri hiyo wamekuwa wakibuni mbinu mbalimbali kuwahadaa wananchi.

Mwaka 2016 Kaimu Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Sanjo Charles Bulugu,alimchongea kwa Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Eliud Mwaiteleke kwa kutoa taarifa za uongo katika mkutano wa Serikali ya Kijiji cha Sanjo akisema  kuwa,Mkurugenzi huyo alishindwa kufika katika mkutano wa kijijinihicho kwa kukosa gari la kumpeleka kusikiliza kero za wananchi hao.

Katika mkutano huo Bulugu alidai kuwa Mkuu wa Wilaya ya Misungwi alitoa agizo akimtaka Mkurugenzi kufika katika kijiji hicho kufuatia malalamiko yaliyotolewa na wananchi wa Kijiji cha Sanjo kwa kuuomba Uongozi wa Wilaya ya Misungwi ufike hapo kusikiliza kero zao.

Katika taarifa hiyo iliyotengenezwa ili kuwahadaa wananchi wa Kijiji cha Sanjo Bulugu alimsingizia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Misungwi Eliud Mwaiteleke kuwa eti
amekwama kufika katika mkutano huo kutokana na kukosa usafiri kufuatia gari lake kuwepo katika usimamizi wa mitihani ya Taifa kwa wanafunzi wa Darasa la Saba.

“Ndugu zangu wananchi kwa niaba ya Mkurugenzi  napenda kuwaomba radhi kwa kuchelewa kufika hapa mgeni wetu sasa ni saa tano asubuhi ,ni kwamba mgeni wetu hataweza kufika kutokana na kukosa usafiri wa kumleta hapa,gari lake liko kwenye shughuli za Mitihani ya Darasa la saba”alisema Bulugu huku miguno na maswali toka kwa wananchi vikitawala.

“Hivi Mtendaji huoni kuwa huu ni uzembe wa makusudi,magari yote ya Halmashauri hayapo kweli? hata gari lake liko kwenye mitihani?mbona hawa watu wanataka kuturudisha tulikotoka? Sasa tunakuagiza Mtendaji ukamwambie Mkuu wa Wilaya kuwa agizo lake limepuuzwa! kwa nini Mkurugenzi asitumie hata Hiece?” alihoji mmoja wa wananchi waliokuwepo katika mkuitano huo.
Yaliyojiri baada ya Uchunguzi

Uchunguzi uliofanywa kipindi hicho Tanzania Daima lilibaini kuwa, taarifa hizo hazikuwa za kweli kwani Mkurugenzi huyo alikuwa safari ya kikazi Mjini Dodoma.
taarifa hiyo iliwakera wananchi na kuahidi kugomea mikutano ijayo iwapo hawatapata maelezo ya kutosha juu ya tukio hilo ambapo hadi leo hii wananchi hao hawajawahi kusikilizwa kutokana na kwamba mkutano huo ulikuwa kama kiini macho kuficha tuhuma zilizokuwepo kwa watumishi kipindi hicho.

Mwandishi wa Tanzania Daima alimtafuta Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi  ili kutolea ufafanuzi wa taarifa iliyotolewa na Afisa Mtendaji huyo ambapo Mkurugenzi alisema kuwa hazina ukweli.
“Mimi kwa sasa niko Mbeya,nimeshtushwa sana na taarifa hizo mimi nikose usafiri si ningeenda na pikipiki? Sisi kazi yetu ni moja tu nayo ni kuwatumikia wananchi na si vinginevyo sijui Mtendaji huyo kapata wapi maelekezo hayo ngoja nifuatilie”alisema Mwaiteleke.

Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti wananchi hao walisema kuwa wamekwazwa na kitendo cha Mkurugenzi kushindwa kufika kijijini jambo walilosema bila kumung’unya maneno kwamba ni uzembe.

Akiweka wazi siri zilizokuwa zimefichika katika maandalizi ya taarifa za uongo zilizotolewa na Kaimu Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Sanjo Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyasubi Meni Lutandula aliliambia Tanzania Daima  kuwa kuna udanganyifu mkubwa katika ujenzi wa tenki la maji katika kijiji cha Sanjo ambapo walibaini matumizi mabaya ya fedha za wananchi kiasi cha shilingi milioni 20,828,502;60 katika ujenzi wa mradi wa maji.

“Inasikitisha kuna ujenzi wa shule ambayo hata hivyo ilikuwa haijaanza kufanya kazi lakini tayari vyumba vimechakaa kutokana na kujengwa chini ya kiwango wananchi kulazimishwa kuchangia shilingi 6500 kila familia kwa ajiri ya ukarabati wa vyumba hivyo”.alisema Lutandula.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Sanjo Bukali John alipotakiwa kutolea ufafanuzi sakata la ujenzi wa madarasa chini ya kiwango alisema alikiri na kumuonya mwandishi asiripoti taarifa hizo.
“Nisingependa uendelee kufuatilia jambo hilo kwa kuwa wananchi tayari tumeshawashawishi wananchi na wamekubali kuchangia fedha kwa ajiri ya kurekebisha vyumba hivyo ni kweli kuna mapungufu yaliyojitokeza katika ujenzi wa vyumba hivyo lakini sitaki ufuatilie suala hilo maana tayari tumeshafanya vikao na wananchi na tumekubaliana wachangie fedha kiasi cha shilingi 6500 kila familia ili tuweze kukarabati vyumba hivyo” alisema Bukali.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Juma Sweda alipotafutwa kuzungumzia kama alitoa agizo kwa Mkurugenzi ambapo alisema kuwa hana taarifa zozote juu ya agizo hilo na kwamba yeye hajawahi kufanya ziara katika kijiji cha Sanjo.
“Mimi sijawahi kufanya ziara yoyote katika kijiji hicho isipokuwa nilishiriki kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Fela hivyo sijui Afisa Mtendaji huyo alitoa wapi maelekezo hayo nitafuatilia kujua zaidi juu ya jambo hilo”alisema Sweda.
Baraza la Madiwani kuwapa Siku 30 kwa watendaji

Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, limewapa muda wa siku 30 watendaji kushughulikia suala la makusanyo ya mapato ya ndani na utekelezaji wa mradi wa maji katika kijiji cha Fela uliokwama tangu 2013.

Azimio hilo lilipitishwa na baraza hilo wakati wa kikao kilichofanyika mjini Misungwi juzi, baada ya kubainika kuwa hadi Desemba 2017 halmashauri hiyo imekusanya Sh734.9 milioni pekee kati ya malengo ya kukusanya Sh2.06 bilioni.

Katika Baraza hilo Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga aliwacharukia watendaji na kuwataka watoe  maelezo juu ya kusuasua kwa ukusanyaji mapato, hali inayokwamisha utekelezaji wa miradi.

Akitolea mfano wa kusuasua alisema kuwa katika mwalo huko Mbarika vitabu vya halmashauri vinaonyesha hakuna mapato yanayokusanywa, lakini hivi karibuni kamati ya uchumi na mipango ilipotembelea eneo hilo ilifanikiwa kukusanya Sh15,000 kwa muda mfupi, hali inayodhihirisha udhaifu katika ukusanyaji wa mapato.

Kuhusu mradi wa maji wa Fella ambao utekelezaji wake ulianza Juni 2013 na kutakiwa kukamilika Desemba mwaka huo, baraza limempa siku 30 mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Eliud Mwaiteleke kuhakikisha unakamilika na kutoa maji au uwekwe chini ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Mradi huo ambao tayari umegharimu zaidi ya Sh644 milioni, unatarajiwa kunufaisha wakazi 6,473 wa vijiji vya Fella, Ngeleka na Bujingwa.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, mhandisi wa maji wa halmashauri hiyo, Ali Mruma alisema tayari maji yameanza kutoka na zinahitajika zaidi ya Sh3.8 milioni kununulia mashine ya kuyasukuma ili kuongeza usambazaji wa huduma kwa wananchi.

Diwani wa viti maalum, Christina Nyanda alisema maji hayo kata ya Mamaye yanatoka kwa kusuasua na kutaka wataalamu kutoa maelezo sahihi.

Mkandarasi wa kampuni ya COWI Tanzania Ltd inayotekeleza mradi huo, Ernest Tinka alikiri kuwapo upungufu na kuahidi kurekebishwa.

Siri zilizofichika nyuma ya miradi Misungwi.

1.      Kuna maslahi binafsi katika utekelezaji wa Miradi mbalimbali Wilayani Misungwi kutokana na baadhi ya viongozi wa Serikali na kisiasa kudaiwa kuwa ndiyo wamiliki wa makampuni yanayotekeleza miradi hiyo ambapo kwa haya aliyokutana nayo Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Suluhisho kuinusuru Miradi ya maendeleo dhidi ya Mchwa.
inatakiwa kuunda Tume Maalumu kwa ajiri ya kuchunguza ufujaji wa mali za Umma lakini pia watumishi wa Wilaya ya Misungwi wahamishwe kutokana na Mtandao wao unaokwamisha kujulikana kwa uozo kupitia kwa Kaimu Afisa Habari wa Wilaya ya Misungwi Thomas Lutego ambaye hata akiwa na shughuli hubagua Waandishi wa Habari kwa lengo la kuficha maovu hayo.