Wednesday, November 2, 2016

CAG abainisha Madudu Misungwi


Na Antony Sollo Misungwi

MZIMU wa Hati yenye Mashaka umezidi kuiandama Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi,hii ni baada ya ripoti iliyotolewa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za Serikali CAG kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2014/15.

Kufuatia ripoti ya CAG,Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi imepata Hati yenye Mashaka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo Halmashauri hiyo kudaiwa madeni na watu mbalimbali yanayofikia shilingi 472,018,814.

Hoja zingine za ukaguzi zilizotolewa katika ripoti ya CAG ni kuwepo kwa malipo ya mishahara yaliyofanywa kwa watumishi waliokoma utumishi ( hewa )walioisabishia Serikali kiasi cha shilingi 12,483,000,ununuzi wa mafuta hewa kiasi cha shilingi 43,399,972,ununuzi wa mafuta kwa ajiri ya magari binafsi kwa kutumia mwamvuli wa Serikali shilingi 7,815.450.

Ripoti hiyo pia imeonyesha utekelezaji wa miradi ya maji ya bomba ambayo imeigharimu Halmashauri hiyo mamilioni ya shilingi kama ifuatavyo,mradi wa maji ya bomba Ngaya/Matale shilingi 305,058,000,mradi wa maji ya bomba kijiji cha Bujingwa shilingi 293,590,000.

Kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji ya bomba tayari Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Juma Sweda amefanya ziara ya kushtukiza katika maeneo mbalimbali na kubaini madudu hayo na kuagiza taasisi mbalimbali likiwemo Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Takukuru kufanya Uchunguzi hatimaye wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kufikishwa Mahakamani.

Kufuatia madudu hayo, Diwani wa Kata ya Mabuki Nicodemus Ihano ( CCM ) alisimama na kuhoji kuhusu mapungufu ya taarifa mbalimbali zilizotolewa katika baraza lililokaa 18 August mwaka huu lakini alitolewa nje ya ukumbi wa Mkutano na Mwenyekiti wa Halmashauri  ya Wilaya ya Misungwi Antony Bahebe kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Kiongozi mmoja kutoka ndani ya CCM aliwaambia Mwandishi wa Habari hizi kuwa kuna udanganyifu mkubwa uliofanyika wakati wa upatikanaji wa tenda na utekelezaji wa  ujenzi wa miradi ya maji huku Mbunge wa Jimbo la Misungwi Charles Kitwanga akihusishwa kuwa na maslahi katika miradi hiyo.

“kuna tatizo kubwa juu ya upatikanaji wa Mkandarasi wa Mradi wa maji kwani Mbunge alileta Kampuni moja kutoka Dar es salaam ambayo mmiliki wake wana urafiki,si hivyo tu hata Mwenyekiti wetu wa Halmashauri ya Wilaya Antony Bahebe ndiye msimamizi wa mradi ambapo tunashangazwa na vitendo vya viongozi hawa kujiingiza katika kusimamia kampuni kwa maslahi binafsi”alisema kiongozi huyo ambaye hata hivyo hakutaka kuandikwa jina lake kwenye gazeti.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi  Eliud Mwaiteleke alipotafutwa kuzungumzia ripoti hiyo alisema kuwa yuko msibani hivyo yafanyike mawasiliano kwa ujumbe mfupi wa maandishi ambapo hata hivyo alijibu kwa hasira kuwa hana majibu juu ya ripoti hiyo

Kwa upande wake Mbunge wa JImbo la Misungwi Charles Kitwanga alipotafutwa kwa njia ya simu simu yake iliita bila majibu hata pale alipotumiwa ujumbe mfupi hakujibu chochote na baadaye simu yake ilizimwa.