· Wasema iliacha
kuangalia matatizo ya wananchi
· Ilienda kwa ajili
ya kuangalia madini pekee.
· Wasema huo si
uzalendo,Utaifa.
· Kamati hiyo
haikufanyi kazi Mgodi wa Elhilal ulioko hapo
Na Antony Sollo Shinyanga.
09.09.2017
WANANCHI wa Mji mdogo wa Maganzo Wilayani Kishapu Mkoa wa
Shinyanga wametoa maoni yao kuhusu ripoti iliyowasilishwa kwa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli huku wakiiponda Kamati
iliyoundwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai
wakisema Kamati hiyo ina mapungufu makubwa Tanzania Daima limeelezwa.
Akizungumza na gazeti hili mmoja wa wahanga wa mgodi huo George
Joseph ambaye alipigwa risasi na walinzi wa mgodi huo ameilalamikia Kamati hiyo
kwa kushindwa kuangalia maisha ya Raia na badala yake Kamati hiyo imedaiwa
kujikita zaidi kuangalia wizi wa Madini ya Almasi katika Mgodi mmoja huku Mgodi
unaomilikiwa na Phantom ambaye anamiliki Kampuni ijulikanayo kama Elhilal
Mining ukiachwa bila kuchukuliwa taarifa zake yakiwemo mauaji ya wananchi
wakazi wa Maganzo.
“ Ripoti ya Kamati hii ina mapungufu makubwa sana kwani ujio
wake haukulenga kukutana na wahanga na pia ilipata makengeza kwa kushindwa
kuuona mgodi wa Elhilal Mining unomilikiwa na Pantom ambapo Kamati hiyo
imekutana na watu ambao taarifa zao zimejikita kwenye madini pekee lakini
haikukumbuka kama kuna matukio makubwa ya Mauaji, unyanyasaji wa raia kama
ilivyokuwa katika Kamati iliyoundwa kuchunguza zoezi la Operation Tokomeza
ambapo Kamati hiyo ilizama zaidi katika masuala ya Haki za Binadamu kujua
matatizo yiyowapata raia”alisema George.
George ameeleza kusikitishwa kwake na ubaguzi uliofanywa na Mkuu
wa Wilaya ya Kishapu Nyabaganga Talaba kwa kuwazuia waathirika waliopigwa
risasi na walinzi wa Mgodi wa Mwadui kuingia katika kikao cha Kamati hiyo ili
kueleza hali halisi na yanayojili kila siku katika Mgodi wa Mwadui na kwamba
eneo la Mgodi wa Mwadui halimilikiwi na WDL pekee bali kuna mwekezaji mwingine
ambaye amekuwa tishio kwa usalama wa raia kutokana na kuua vijana wengi na haku
akilindwa na viongozi wa Serikali na hadi sasa hakuna hatua zilizochukuliwa
dhidi yake.
“Mwekezaji huyu ameua watu wengi na viongozi wa Jeshi la Polisi
na Madaktari waliokuwepo kipindi cha awamu ya Nne walikuwa na mnyororo mkubwa
wa rushwa ambapo vijana wengi waliuawa na kupelekwa gerezani huku mmiliki wa
Kampuni ya Elhilal akishinikiza vijana wanaokamatwa kupelekwa gerezani na
kuwekwa mahabusu kwa lengo la kutukomoa,Phantom amediliki kunyang’anya maeneo
ya watu lakini Serikali ilikuwa imewekwa mfukoni hebu tumuombe Mh Rais aje
tumweleze mateso tuliyo nayo sisi wananchi wa Maganzo”alisema George.
Kwa mujibu wa George Joseph ambaye ni mmoja wa waathirika
kutokana na kupigwa risasi na walinzi wa mgodi wa Mwadui ni kwamba kuna
makundi mbalimbali yaliyoachwa kusikilizwa na Kamati ya Ndugai na bila kuyataja
makundi hayo ripoti hiyo inakuwa haijakamilika na inakuwa na doa lisilofutika.
Uchunguzi uliofanywa na Mwandishi wa gazeti hili umebaini kuwa
Kamati hiyo ilipata kigugumizi cha kukutana na wahanga waliopata ulemavu
kutokana na kushambuliwa kwa risasi za moto na walinzi wa Kampuni ya Zenity
Security inayolinda rasrimali za mgodi wa Mwadui pamoja na walinzi wa Kampuni
ya Elhilal Mining ambapo baada ya kulalamika sana wahanga hao waliahidiwa na
Kamati hiyo kwamba wangekutana na Wajumbe wa Kamati hiyo Mjini Dodoma kabla ya
kukabidhi Ripoti kwa Rais John Pombe Magufuli na sasa wanajiuliza! kwa kuwa
Kamati hiyo imekabidhi ripoti hiyo bila kuwasikiliza watapata wapi tena nafasi
ya kukutana ili waweze kueleza matatizo yao?
Katika hatua nyingine George na wenzake wamemuomba Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya uchunguzi wa Viongozi wa Jeshi la
Polisi waliokaa muda mrefu Mkoani Shinyanga maana kuna taarifa za kuwepo kwa
namna Fulani ya ushirikiano kati ya taasisi za Serikali na Makampuni
yanayofanya shughuli zake katika eneo la Mwadui.
“ kuna kesi nyingi za mauaji,kujeruhi kwa silaha za moto
zimekuwa zikizimwa muda mrefu kwa ushirikiano wa madaktari wa Hospitali ya
Serikali wakati wa uchunguzi wa majeruhi zikiwemo maiti baada ya mauaji
yanayotokana na walinzi wa mgodi wa Mwadui na Elhilal inayomilikiwa na
Phantom”.alisema George.
Ameyataja makundi hayo kama ifuatavyo.
Waliopigwa risasi na kupata ulemavu wa kudumu.
Katika kundi hili George anasema liko na watu wafuatao, yeye
mwenyewe George Joseph Bwisige (alipigwa risasi na kupelekea kukatwa mguu wa
kulia lakini hadi sasa hakuna hatua zozote zilizochukuliwa),Hamud Said , Marco
Ngussa (ambaye alipigwa risasi na kupasuliwa bandama),Nyalulu Sitta (alipigwa
risasi na kutobolewa jicho),
Kundi lingine ni la watu waliouawa kwa kupigwa risasi na Askari
wa mgodi.
Hawa ni Benard Edward maarufu (Mayo), Shilagi Masali mkazi wa
Masagala,Jishosha Daud, Hamad Shunda Mkazi wa Ikonongo ambaye hakuonekana
isipokuwa nguo zake pekee tu ndiyo zilizoonekana
Hawa ni kundi dogo tu ambao taarifa zao zimeweza kupatikana na
wengi wamepotelea katika mashimo yenye kina kirefu baad ya kukimbizwa
wakielekezwa huko kwa lengo la kuwaua na wanamuomba Rais Magufuli aweze
kuangalia utaratibu unaofaa ili kuwapatia kifut jasho waweze kukidhi mahitaji
ya kibinadamu maana wamefanyiwa ukatili usiowezakusahaulika maishani mwao.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
amekabidhiwa Ripoti Maalumu ya kuchunguza Biashara ya Madini ya Almasi na
Tanzanite nchini 7 Agosti 2017 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Kassim Majaliwa tukio lililofanyika katika viwanja vya Ikulu jijini
Dar es Salaam.
Kabla ya kukabidhiwa Ripoti hizo kwa Rais Magufuli na
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Spika wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai alizipokea ripoti hizo kutoka kwa
Wenyeviti wa Kamati Maalumu alizoziunda ambazo zilijumuisha Wabunge wa Bunge la
Tanzania kutoka vyama mbalimbali vya Siasa.
Kamati hizo ziliongozwa na Dotto Biteko aliyeongoza Kamati ya
kuchunguza biashara ya Madini ya Tanzanite na Mussa Azzan Zungu Kamati ya
kuchunguza biashara za Madini ya Almas.
Kamati hizo ziliundwa wakati wa Mkutano wa Saba wa Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kuchunguza mfumo bora wa
uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa biashara ya madini ya Almas na
Tanzanite.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa ripoti hizo, Rais Magufuli
amemtaka Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwaita Wataalamu na
Taasisi zote zinazohusika na masuala ya madini kufanya maandalizi ya kubadili
Sheria zitakazosaidia Taifa kunufaika na rasilimali zake za madini.
“ Huu ndiyo wakati wa kubadilisha sheria zetu. Mhe, Waziri
Mkuu uwaite Wataalam wote wanaohusika na madini maandalizi haya yaanze haraka,”
amesema Dkt. Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amesisitiza suala la uzalendo kwa
Watanzania wote katika kusimamia rasilimali za nchi na kusema kuwa, ikiwa
watanzania wataweka mbele uzalendo Taifa litasimama na kwamba hatutochezewa na
wawekezaji tena na mikataba mibovu ambayo italiingizia Taif letu hasara.
Dkt. Magufuli amesema hivi sasa uchumi wa Tanzania unakua kwa
asilimia 7 hadi 7.1 na nchi ya nne nyuma ya nchi ya Ethiopia ambayo uchumi wake
unakua kwa asilimia 8.3 na kueleza kuwa, iwapo rasilimali hizo zingesimamiwa
vizuri taifa lingenufaika zaidi na kuwa na uchumi zaidi ya nchi ya India ambayo
haizalishi madini ya Tanzanite lakini imekuwa ni muuzaji mkubwa wa madini hayo.
“ Tutangulize maslahi ya nchi yetu mbele,nataka tufike
mahali tuanze upya,Mhe. Spika muendelee kutusaidia katika kusimamia rasilimali
zetu, amesema Dkt. Magufuli.”
Katika hatua nyingine Rais Dkt. John Pombe Magufuli amewataka
Wateule waliotajwa katika ripoti hiyo kukaa pembeni ili kupisha vyombo vya
Ulinzi na Usalama kufanya kazi yake vizuri.
Rais Magufuli amesema hayo yote yanafanyika ili kuh akikisha
kwamba watanzania wananufaika na rasilimali hizo na kueleza kuwa, bado
watanzania hawajanuifa vya kutosha na rasilimali za nchi ikilinganishwa na
rasilimali zilizopo.
Awali, akizungumza wakati wa kukabidhi Ripoti hizo, Waziri Mkuu
Majaliwa alisema kuwa, Kamati mbili zilizoundwa na Spika wa Bunge zimefanya
kazi kubwa na hali hiyo inatokana nia ya dhati aliyoionyesha Rais Magufuli
kuhakikisha,rasilimali za madini zinakuwa na tija kwa Taifa.
Kwa upande wake Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Job Ndugai alisema kuwa, Bunge liko tayari kuzipitia na kuzifanyia
marekebisho Sheria zote ambazo hazilinufaishi Taifa na kueleza kuwa ipo haja ya
kulifanyia kazi suala la mifumo ya udhibiti wa rasilimali hizo.
Ndugai amewataka viongozi wa Serikali waliopewa dhamana ya
kusimamia shughuli za Umma kuguswa na umaskini wa Watanzania na hivyo kuzitaka
Bodi mbalimbali nchini kubadilika na kuona haja ya kuangalia na kufuatilia kwa
karibu maeneo wanayoyasimamia.
Akiwasilisha ripoti ya Madini ya Almasi Mwenyekiti wa Kamati
hiyo Mussa Azzan Zungu alisema soko la madini ya Almasi bado liko katika
kiwango duni japokuwa Almas yenye thamani ya juu inapatikana Tanzania pekee.
a
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Tanzanite Dotto
Biteko alieleza kuwa, asilimia 80 ya Tanzanite inatoroshwa nchini na asilimia
20 ya madini hayo ndiyo yanayoingia katika mfumo wa kodi nchini.
MWISHO.