Monday, February 27, 2017

Wanafunzi Buhongwa B wasomea chini ya mti.




Na Antony Sollo Mwanza

WANAFUNZI wa Shule ya Msingi Buhongwa B iliyoko katika Jimbo la Nyamagana Mkoani Mwanza wanasoma wakiwa chini ya mti wakiwa hawana hata Madawati ya kukalia kufuatia changamoto kubwa za Vyumba vya Madarasa Matundu ya vyoo na nyumba za walimu zinazoikabili shule hiyo Tanzania Daima limebaini.

Mwandishi wa Tanzania Daima aliyefika shuleni hapo alishuhudia wanafunzi zaidi ya mia moja wakisomea nje chini ya miti huku kukiwa na wingu zito la mvua  ambapo baada ya kufuatilia kwa wahusika kujua tatizo ni nini walimu wa shule waligoma kueleza chochote na kumuomba Mwandishi huyo akaonane na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Kiomoni Kibamba kwa kuwa yeye ndiye msemaji mkuu.

Mwandishi wa gazeti hili alimtafuta Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza kuzungumzia suala hilo ambapo alikiri kuwepo kwa upungufu mkubwa wa vyumba vya Madarasa.

“Tuna changamoto kubwa ya vyumba vya Madarasa hii inatokana na idadi kubwa ya wanafunzi ambapo kwa mwaka 2016 tuliandikisha wanafunzi 500 na mwaka 2017 hadi jana 27 feb tumeandikisha wanafunzi 450 jumla ya wanafunzi wote kwa sasa ni 950 katika Shule hiyo”alisema Kibamba.

Akifafanua Mikakati waliyo nayo Mkurugenzi huyo alisema kuwa Mwaka 2016 waliandikisha wanafunzi  8000 katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana na mwaka 2017 kuna wanafunzi zaidi ya 8000 ambapo mpango wa Elimu bure ulitangazwa na Rais Magufuli umesababisha ongezeko kubwa la wanafunzi na kuvuka malengokatika uandikishaji wa wanafunzi.

Hadi Sasa Serikali imepeleka Shilingi mil 15,000,000 katika Shule hiyo kwa ajiri ya ujenzi wa vyumba vya madarasa huku Shilingi Mil 900,000,000 zikipelekwa Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana ajiri ya kukamilisha mradi wa madawati ya akiba ili kukabiliana na ongezeko lolote litakalojitokeza baada ya kukamilika kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa shuleni hapo

Kwa upende wake Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Stanslaus Mabula alikiri kuwepo kwa changamoto zinazoikabili shule hiyo ambapo Mabula alisema kuwa ni kweli kuna upungufu mkubwa wa vyumba vya Madarasa, Nyumba za walimu, matundu ya vyoo pamoja na majengo ya Ofisi za Walimu.

“Tuna uhaba mkubwa wa vyumba vya madarasa katika jimbo letu la Nyamagana lakini pamoja na hayo tumejitahidi kwa upande wa Madawati tumefanikiwa kukamilisha idadi inayotakiwa na hadi sasa tuna ziada ya madawati 3000 yakiwa hayana pa kuyaweka.

Akizungumzia mikakati waliyonayo kukabiliana na changamoto hizo Mbunge huyo alisema kuwa wanahamasisha wadau mbalimbali ikiwemo Serikali kuu pamoja na wananchi katika maeneo mbalimbali jimboni humo kuchangia ujenzi wa vyumba vya Madarasa vipatavyo 24 ili kuweza kuanzisha Shule mpya kupunguza mrundikano wa wanafunzi katika shule mbalimbali jimboni humo.

“Tuna upungufu wa vyumba vya Madarasa vipatavyo 1200 na hadi sasa tunaendelea kuhamasisha wadau mbalimbali kuchangia ujenzi wa vyumba vya Madarasa vipatavyo 24 kwa ajiri ya kuanzisha Shule mpya ili kupunguza mrundikano wa wanafunzi katika shule mbalimbali katika jimbo letu”.alisema Mabula.

MWISHO