Saturday, January 20, 2018

Kushamiri kwa Migogoro ya Ardhi Nchini



Makala:

Zikiwa zimepita siku chache tangu vikao vya Kamati za Bunge vianze mjini Dodoma hali ya mambo katika maeneo mbalimbali nchini si shwari kwani kumezuka mijadala mikubwa kutokana na madhira yaliyowapata wananchi kutokana na kupigwa,kuporwa mali ,kujeruhiwa kwa risasi za moto na Askari wakati wa utekelezaji wa operesheni za kuwaondoa wananchi wanaokaa katika maeneo yanayodaiwa kuwa ni Hifadhi pamoja na Ardhi inayodaiwa kutengwa kwa ajili ya Uwekezaji nk.

Vikao hivyo vilianza jumatatu ya tarehe 15 januari 2018,hii ikiwa ni kabla ya kuanza kwa Mkutano wa kumi wa Bunge,shughuli zilizopangwa kutekelezwa katika kipindi cha vikao hivi ni pamoja na ziara za ufuatiliaji ,uchambuzi wa miswada mbalimbali na kupokea maoni ya wadau pamoja na kupokea taarifa za utendaji za Wizara.

Kamati tatu za kisekta ambazo zitakuwa na jukumu la uchambuzi wa miswada mbalimbali ni pamoja na Kamati ya Sheria,Kamati ya Ardhi,Maliasili na Utalii pamoja na Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Maoni yangu kwa wadau na wajumbe wa Kamati hizi watumie muda huu kuangalia namna ya kutatua tatizo lililomuelemea Mheshimiwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi  Wiliam Lukuvi ambaye kama angekuwa si Kiongozi Mahiri huenda Rais Magufuli angekuwa ameshamuweka pembeni kutokana na malalamiko likuki yanayoiandama Ofisi (Wizara)yake.

Kipekee niwapongeze Mawaziri hawa wawili Mheshimiwa Wiliam Lukuvi na Naibu wake Mheshimiwa Angelina Mabula kwa kazi kubwa wanayofanya ikiwemo kupokea na kufanyia kazi malalamiko takribani nchi nzima.

Ukweli Wizara hii ni ngumu,ina mianya mingi ya rushwa ambayo kama si umahiri wa Mawaziri hawa huenda Mahakama na Mabaraza ya ardhi kungefurika mafaili ya malalamiko zaidi ya haya,lakini kutokana na uchunguzi nilioufanya naona kabisa na ninaweka bayana kuwa Mawaziri hawa wamejitoa muhanga kwa ajili ya kupigania haki za wananchi wanyonge.


katika mkutano wa tisa wa bunge la kumi na moja November 16, 2017 akijibu maswali ya papo kwa papo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhshimiwa Khasim Majaliwa aliulizwa maswali na wabunge Magdalena Sakaya (Kaliua) aliyetaka kujua Serikali imejipangaje kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi suala ambalo ni la kidunia.

Katika majibu yake Waziri Mkuu alisema,
“Mheshimiwa Spika,mabadiliko ya tabia nchi yaliyokumba dunia na Tanzania ikiwemo,tunaendelea kukabili changamoto kwa  kuweka mipango mbalimbali kuhakikisha kuwa tunakabiliana na mabadiliko hayo,moja ya mikakati hiyo ni kusimamia Sheria ya uhifadhi wa Mazingira ili kuhakikisha Mazingira yanabaki yanasaidia kufanya mabadiliko ya hali ya hewa ya nchi yanabaki kuwa ya kawaida yanayowezesha binadamu au viumbe hai vyote ndani ya nchi kufanya kazi zake vizuri na kupata mahitaji yake vizuri”

Waziri Mkuu pia alisema kuwa Serikali imeendelea kusimamia Sheria za mazingira ambazo pia zinakinga maeneo mbalimbali hii ni pamoja na misitu,mito na maeneo mengine yote ili kukabiliana na hali hiyo.

Serikali pia imeendelea kutoa elimu kwa jamii kuwaelimisha Watanzania umuhimu wa Kutunza mazingira yetu kwa ujumla,zikiwemo taasisi za kimataifa zimeendelea pia kusaidia kupambana na tatizo hili.

Waziri Mkuu alitoa wito kwa watanzania nia wote kutunza mazingira na kwamba mabadiliko ya tabia nchi duniani hayatafanikiwa iwapo tutaendelea kuharibu misitu yetu,kuharibu vyanzo vyetu,tunaweza kukosa huduma za jamii zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi,hivyo ni muhimu sana kushirikiana na wataalamu kwa pamoja na wananchi wanaoishi na kila mmoja aliyepewa dhamana katika maeneo yao ili kuweza kushiriki kwa pamoja kuhifadhi Mazingira yetu.

Waziri Mkuu pia aliulizwa swali na Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale (CUF) kuhusu shambulio lililofanywa julai 2017 na Askari Polisi ndani ya msikiti ambapo shambulio hilo lilipelekea kifo cha Shekh Ismail Weta na kuondolewa jicho kwa Shekh Abdalah Nakindabu ambapo Mbunge huyo alitaka kujua kama Serikali ina mpango wa kulipa fidia  kwa watu hao.

Akijibu swali hilo Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema kuwa kwanza sina uhakika kama Askari walimshambulia mtajwa hapo na kumtoa jicho lakini jukumu la vyombo vya dola na Jeshi la Polisi likiwemo ni kulinda usalama wa raia na mali zao,si jukumu la polisi kwenda kumshambulia mtu na hatimaye Serikali ianze kufikiria kumlipa mtu fidia kutokana na shambulio lililofanywa na Askari Polisi na kama kuna Askari yeyote amefanya tendo hilo yeye mwenyewe nje ya majukumu yake ya kazi atachukuliwa hatua kama yeye aliyetenda kosa hilo.

“Serikali haiwajibiki kulipa fidia ikiwa si sehemu ya maagizo na wala si jukumu la majeshi ya vyombo vya dola bali ikithibitika mmoja kati ya watumishi wa vyombo vya dola ametenda kosa hilo na ikathibitika hivyo,yeye mwenyewe atawajibika kuchukuliwa hatua kali na ili kama kutakuwa na kulipa fidia itakuwa ni moja ya adhabu ambayo itatolewa na vyombo vinavyotoa hukumu”.alisisitiza Waziri Mkuu.

“Kwa hiyo Mheshimiwa Spika niseme tu kwamba,Serikali wala vyombo vyake vya dola havilengi kufanya kazi ya kuwatendea makosa wananchi bali ni kuwalinda wananchi pamoja na mali zao kama tulivyojipanga kufanya kazi”alisema Waziri Mkuu.

 Swali lingine ambalo nimelenga kulitumia kuthibitisha mambo yanayoashiria  kushamiri kwa migogoro ya Ardhi nchini liliulizwa mbele ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Ulyankulu Mheshimiwa Kadutu kuhusu kuzuiwa kwa wananchi kufanya shughuli za kilimo na ufugaji huku maeneo hayo yakiwa yamepimwa na vijiji vyake vimeandikishwa na wananchi wakiwa na (GN) Tangazo la Serikali.

Akijibu swali hilo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Khasim Majaliwa alisema nchi yetu ina mapori yaliyohifadhiwa kisheria,yana mipaka yake rasmi kwa mujibu wa Sheria zinazoyalinda,mapori haya yapo katika kila eneo,na ni budi kila mtanzania kushiriki kuyahifadhi,kumetokea uvamizi unaofanywa na waliojirani na maeneo hayo,ni kweli maeneo hayo yamekuwa na migogoro mingi kati ya mapori yetu na vijiji,kati ya mapori na wananchi ambao wanaoenda kufanya shughuli za kijamii huko ndani ambapo pia Serikali hairuhusu kufanyika kwa shughuli za kijamii.

Kutokana na migogoro hii ya muda mrefu,Waziri Mkuu alitoa agizo kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kufanya mapitio ya mipaka na kuweka alama kwenye mipaka ya mapori yote.

Kilichobainika,Serikali ilikuwa imeshasajili vijiji hivyo na kulianza migogoro hiyo baada ya wataalamu walioanza kwenda kufanya kazi ya kubaini mipaka katika mapori hayo tuliwasihi wananchi walio kwenye vijiji vilivyo ndani ya mapori hayo wawaache wataalamu wafanye mapitio na waweke alama hizo zinazobainisha mipaka ya ramani baada ya hapo Serikali itakuja kuona ni kijiji gani kilicho ndani na je pale palipo kijiji malengo yetu ya uhifadhi yamefikiwa na bado ni Mahitaji sahihi ili baadaye tuje kufanya maamuzi ya au kupunguza maeneo ambayo kwa sasa kwa uhifadhi huo hauna tija ili kuondoa migogoro.

Waziri Mkuu alisema kuwa kazi hiyo inaendelea na aliagiza kuwa ifikapo tarehe 30 mwezi wa kumi na mbili 2017 wataalam hao wawe wamekamilisha kupima mapori ambayo bado  baada ya hapo Serikali iangalie ni vijiji vingapi vilisajiliwa na Serikali na viko ndani ya hifadhi/mapori hayo na kama vijiji hivyo bado viko kwenye maeneo yaliyo na tija kwa malengo ya uhifadhi au la ili Serikali itoe maamuzi mengine.

Waziri Mkuu alitoa wito kwa wananchi ambao wako kwenye hifadhi ambazo zimetambuliwa baada ya uwekaji wa alama uliofanywa na wataalam waendelee na kazi hiyo baada ya kazi hiyo Serikali ifanye mapitio na kufanya maamuzi kwa maslahi ya nchiikiwemo kufuta kijiji au kubadilisha mipaka ambapo mpaka hapo Mahusiano kati ya Serikali na wananchi yatakuwa yameenda vizuri na wananchi watashiriki kulinda mapori na hifadhi hizo.  
Nakubaliana na majibu ya Mheshimiwa Waziri Mkuu Khasim Majaliwa,sasa kero zilizoko katika maeneo mbalimbali Nchini ni namna wahusika walioagizwa kufanya kazi hiyo walivyogeuza zoezi hilo kuwa uwanja wa vita!

Iwapo Serikali imeweza kubaini mapungufu yaliyosababishwa na watendaji mbalimbali wa Serikali katika Taasisi zake kikiwemo Chuo Kikuu cha Dar Es salaam kuingia mikataba vivyo hivyo wapo watendaji wa Serikali walioamua kufanya wanayotaka katika agizo hili la Mheshimiwa Waziri Mkuu hivyo ,kamati ya Maliasili ifuatilie maeneo mbalimbali na maeneo ya kuanza nayo iwe ni Mikoa ya Tabora na Katavi ambapo mpaka hivi sasa vikao vya Kamati za Bunge vinavyoendelea vinaweza kuona ni jinsi gani watendaji wakiwemo wateule wa Mheshimiwa Rais walivyofanya unyama kwa wananchi wa maeneo hayo bila huruma kwa kuchoma vyakula,nyumba,na mali mbalimbali za wananchi jambo linalofanya wananchi waingie mgogoro na Serikali bila sababu.

Kuna aibu kubwa juu ya mambo waliyofanyiwa wananchi kwani wananchi wamefikia hatua za kutozwa fedha kiasi cha shilingi laki moja kabla hata ya utaratibu ulioelezewa vizuri na Mheshimiwa Waziri Mkuu ambapo ingefanyika hivyo,wananchi wasingeweza kupata madhara kiasi cha kusababishwa kwa vifo ,majeruhi,upotevu wa mali na kukosa makazi na aibu ni kwa vijiji vilivyosajiliwa.

Kwa kauli nzuri iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kwamba atambue kuwa viongozi wa Serikali ngazi za chini wamekuwa wakifanya vitu vya kushangaza mpaka wananchi wanajiuliza wana haki gani kwa Serikali yao waliyoiweka madarakani ambapo baada ya muda imekuwa ikiwageuka na kuwaona hawana thamani.

Itambulike kwa ujumla wake kwamba katika zoezi la kuweka mipaka maeneo ya mapori hakukuwa na ushirikishwaji kwa wananchi katika mambo haya ikiwemo matumizi bora ya ardhi haukufanyika hivyo yote yaliyofanyika kuhusu utesaji,uporaji na mengine ilikuwa ni hulka kwa wateule wa Rais ambao walilewa madaraka na kuamua kufanya watakavyo jambo lililosababisha familia za wananchi katika maeneo mbalimbali nchini kuishi maisha magumu ikiwamo kutokuwa na makazi,huduma za kijamii nk.

Nashauri viongozi wakuu wa Kitaifa waweke utaratibu mzuri wa kufuatilia maagizo waliyotoa ili kuona utekelezaji maana pindi wanapoondoka katika maeneo hayo viongozi wa chini yao hugeuka miungu watu na kusahau maelekezo waliyopewa.

MWISHO.