Makala:
Zikiwa
zimepita siku chache tangu vikao vya Kamati za Bunge vianze mjini Dodoma hali
ya mambo katika maeneo mbalimbali nchini si shwari kwani kumezuka mijadala
mikubwa kutokana na madhira yaliyowapata wananchi kutokana na kupigwa,kuporwa
mali ,kujeruhiwa kwa risasi za moto na Askari wakati wa utekelezaji wa
operesheni za kuwaondoa wananchi wanaokaa katika maeneo yanayodaiwa kuwa ni
Hifadhi pamoja na Ardhi inayodaiwa kutengwa kwa ajili ya Uwekezaji nk.
Vikao
hivyo vilianza jumatatu ya tarehe 15 januari 2018,hii ikiwa ni kabla ya kuanza
kwa Mkutano wa kumi wa Bunge,shughuli zilizopangwa kutekelezwa katika kipindi
cha vikao hivi ni pamoja na ziara za ufuatiliaji ,uchambuzi wa miswada
mbalimbali na kupokea maoni ya wadau pamoja na kupokea taarifa za utendaji za
Wizara.
Kamati
tatu za kisekta ambazo zitakuwa na jukumu la uchambuzi wa miswada mbalimbali ni
pamoja na Kamati ya Sheria,Kamati ya Ardhi,Maliasili na Utalii pamoja na Kamati
ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.
Maoni
yangu kwa wadau na wajumbe wa Kamati hizi watumie muda huu kuangalia namna ya
kutatua tatizo lililomuelemea Mheshimiwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Wiliam Lukuvi ambaye kama angekuwa
si Kiongozi Mahiri huenda Rais Magufuli angekuwa ameshamuweka pembeni kutokana
na malalamiko likuki yanayoiandama Ofisi (Wizara)yake.
Kipekee
niwapongeze Mawaziri hawa wawili Mheshimiwa Wiliam Lukuvi na Naibu wake
Mheshimiwa Angelina Mabula kwa kazi kubwa wanayofanya ikiwemo kupokea na
kufanyia kazi malalamiko takribani nchi nzima.
Ukweli
Wizara hii ni ngumu,ina mianya mingi ya rushwa ambayo kama si umahiri wa
Mawaziri hawa huenda Mahakama na Mabaraza ya ardhi kungefurika mafaili ya
malalamiko zaidi ya haya,lakini kutokana na uchunguzi nilioufanya naona kabisa
na ninaweka bayana kuwa Mawaziri hawa wamejitoa muhanga kwa ajili ya kupigania
haki za wananchi wanyonge.
katika mkutano wa tisa
wa bunge la kumi na moja November 16, 2017 akijibu maswali ya papo kwa papo Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhshimiwa Khasim Majaliwa aliulizwa
maswali na wabunge Magdalena Sakaya (Kaliua) aliyetaka kujua Serikali
imejipangaje kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi suala ambalo ni
la kidunia.
Katika majibu yake
Waziri Mkuu alisema,
“Mheshimiwa
Spika,mabadiliko ya tabia nchi yaliyokumba dunia na Tanzania
ikiwemo,tunaendelea kukabili changamoto kwa kuweka mipango mbalimbali kuhakikisha kuwa
tunakabiliana na mabadiliko hayo,moja ya mikakati hiyo ni kusimamia Sheria ya
uhifadhi wa Mazingira ili kuhakikisha Mazingira yanabaki yanasaidia kufanya
mabadiliko ya hali ya hewa ya nchi yanabaki kuwa ya kawaida yanayowezesha
binadamu au viumbe hai vyote ndani ya nchi kufanya kazi zake vizuri na kupata
mahitaji yake vizuri”
Waziri Mkuu pia alisema
kuwa Serikali imeendelea kusimamia Sheria za mazingira ambazo pia zinakinga
maeneo mbalimbali hii ni pamoja na misitu,mito na maeneo mengine yote ili
kukabiliana na hali hiyo.
Serikali pia imeendelea
kutoa elimu kwa jamii kuwaelimisha Watanzania umuhimu wa Kutunza mazingira yetu
kwa ujumla,zikiwemo taasisi za kimataifa zimeendelea pia kusaidia kupambana na
tatizo hili.
Waziri Mkuu alitoa wito
kwa watanzania nia wote kutunza mazingira na kwamba mabadiliko ya tabia nchi
duniani hayatafanikiwa iwapo tutaendelea kuharibu misitu yetu,kuharibu vyanzo
vyetu,tunaweza kukosa huduma za jamii zinazotokana na mabadiliko ya tabia
nchi,hivyo ni muhimu sana kushirikiana na wataalamu kwa pamoja na wananchi
wanaoishi na kila mmoja aliyepewa dhamana katika maeneo yao ili kuweza
kushiriki kwa pamoja kuhifadhi Mazingira yetu.
Waziri Mkuu pia
aliulizwa swali na Mheshimiwa Vedasto Edgar Ngombale (CUF) kuhusu shambulio
lililofanywa julai 2017 na Askari Polisi ndani ya msikiti ambapo shambulio hilo
lilipelekea kifo cha Shekh Ismail Weta na kuondolewa jicho kwa Shekh Abdalah
Nakindabu ambapo Mbunge huyo alitaka kujua kama Serikali ina mpango wa kulipa
fidia kwa watu hao.
Akijibu swali hilo
Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema kuwa kwanza sina uhakika kama Askari
walimshambulia mtajwa hapo na kumtoa jicho lakini jukumu la vyombo vya dola na
Jeshi la Polisi likiwemo ni kulinda usalama wa raia na mali zao,si jukumu la
polisi kwenda kumshambulia mtu na hatimaye Serikali ianze kufikiria kumlipa mtu
fidia kutokana na shambulio lililofanywa na Askari Polisi na kama kuna Askari yeyote
amefanya tendo hilo yeye mwenyewe nje ya majukumu yake ya kazi atachukuliwa
hatua kama yeye aliyetenda kosa hilo.
“Serikali haiwajibiki
kulipa fidia ikiwa si sehemu ya maagizo na wala si jukumu la majeshi ya vyombo
vya dola bali ikithibitika mmoja kati ya watumishi wa vyombo vya dola ametenda
kosa hilo na ikathibitika hivyo,yeye mwenyewe atawajibika kuchukuliwa hatua
kali na ili kama kutakuwa na kulipa fidia itakuwa ni moja ya adhabu ambayo itatolewa
na vyombo vinavyotoa hukumu”.alisisitiza Waziri Mkuu.
“Kwa hiyo Mheshimiwa
Spika niseme tu kwamba,Serikali wala vyombo vyake vya dola havilengi kufanya
kazi ya kuwatendea makosa wananchi bali ni kuwalinda wananchi pamoja na mali
zao kama tulivyojipanga kufanya kazi”alisema Waziri Mkuu.
Swali lingine ambalo nimelenga kulitumia kuthibitisha
mambo yanayoashiria kushamiri kwa
migogoro ya Ardhi nchini liliulizwa mbele ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na Mbunge wa Ulyankulu Mheshimiwa Kadutu kuhusu kuzuiwa kwa
wananchi kufanya shughuli za kilimo na ufugaji huku maeneo hayo yakiwa yamepimwa
na vijiji vyake vimeandikishwa na wananchi wakiwa na (GN) Tangazo la Serikali.
Akijibu swali hilo
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Khasim Majaliwa alisema nchi yetu ina mapori
yaliyohifadhiwa kisheria,yana mipaka yake rasmi kwa mujibu wa Sheria zinazoyalinda,mapori
haya yapo katika kila eneo,na ni budi kila mtanzania kushiriki
kuyahifadhi,kumetokea uvamizi unaofanywa na waliojirani na maeneo hayo,ni kweli
maeneo hayo yamekuwa na migogoro mingi kati ya mapori yetu na vijiji,kati ya
mapori na wananchi ambao wanaoenda kufanya shughuli za kijamii huko ndani
ambapo pia Serikali hairuhusu kufanyika kwa shughuli za kijamii.
Kutokana na migogoro hii
ya muda mrefu,Waziri Mkuu alitoa agizo kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kufanya
mapitio ya mipaka na kuweka alama kwenye mipaka ya mapori yote.
Kilichobainika,Serikali
ilikuwa imeshasajili vijiji hivyo na kulianza migogoro hiyo baada ya wataalamu
walioanza kwenda kufanya kazi ya kubaini mipaka katika mapori hayo tuliwasihi wananchi
walio kwenye vijiji vilivyo ndani ya mapori hayo wawaache wataalamu wafanye
mapitio na waweke alama hizo zinazobainisha mipaka ya ramani baada ya hapo
Serikali itakuja kuona ni kijiji gani kilicho ndani na je pale palipo kijiji
malengo yetu ya uhifadhi yamefikiwa na bado ni Mahitaji sahihi ili baadaye tuje
kufanya maamuzi ya au kupunguza maeneo ambayo kwa sasa kwa uhifadhi huo hauna
tija ili kuondoa migogoro.
Waziri Mkuu alisema kuwa
kazi hiyo inaendelea na aliagiza kuwa ifikapo tarehe 30 mwezi wa kumi na mbili
2017 wataalam hao wawe wamekamilisha kupima mapori ambayo bado baada ya hapo Serikali iangalie ni vijiji
vingapi vilisajiliwa na Serikali na viko ndani ya hifadhi/mapori hayo na kama
vijiji hivyo bado viko kwenye maeneo yaliyo na tija kwa malengo ya uhifadhi au
la ili Serikali itoe maamuzi mengine.
Waziri Mkuu alitoa wito kwa wananchi ambao wako kwenye hifadhi
ambazo zimetambuliwa baada ya uwekaji wa alama uliofanywa na wataalam waendelee
na kazi hiyo baada ya kazi hiyo Serikali ifanye mapitio na kufanya maamuzi kwa
maslahi ya nchiikiwemo kufuta kijiji au kubadilisha mipaka ambapo mpaka hapo
Mahusiano kati ya Serikali na wananchi yatakuwa yameenda vizuri na wananchi
watashiriki kulinda mapori na hifadhi hizo.
Nakubaliana na majibu ya
Mheshimiwa Waziri Mkuu Khasim Majaliwa,sasa kero zilizoko katika maeneo
mbalimbali Nchini ni namna wahusika walioagizwa kufanya kazi hiyo walivyogeuza
zoezi hilo kuwa uwanja wa vita!
Iwapo Serikali imeweza
kubaini mapungufu yaliyosababishwa na watendaji mbalimbali wa Serikali katika
Taasisi zake kikiwemo Chuo Kikuu cha Dar Es salaam kuingia mikataba vivyo hivyo
wapo watendaji wa Serikali walioamua kufanya wanayotaka katika agizo hili la
Mheshimiwa Waziri Mkuu hivyo ,kamati ya Maliasili ifuatilie maeneo mbalimbali
na maeneo ya kuanza nayo iwe ni Mikoa ya Tabora na Katavi ambapo mpaka hivi
sasa vikao vya Kamati za Bunge vinavyoendelea vinaweza kuona ni jinsi gani watendaji
wakiwemo wateule wa Mheshimiwa Rais walivyofanya unyama kwa wananchi wa maeneo
hayo bila huruma kwa kuchoma vyakula,nyumba,na mali mbalimbali za wananchi
jambo linalofanya wananchi waingie mgogoro na Serikali bila sababu.
Kuna aibu kubwa juu ya
mambo waliyofanyiwa wananchi kwani wananchi wamefikia hatua za kutozwa fedha kiasi
cha shilingi laki moja kabla hata ya utaratibu ulioelezewa vizuri na Mheshimiwa
Waziri Mkuu ambapo ingefanyika hivyo,wananchi wasingeweza kupata madhara kiasi
cha kusababishwa kwa vifo ,majeruhi,upotevu wa mali na kukosa makazi na aibu ni
kwa vijiji vilivyosajiliwa.
Kwa kauli nzuri
iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kwamba atambue kuwa viongozi wa
Serikali ngazi za chini wamekuwa wakifanya vitu vya kushangaza mpaka wananchi wanajiuliza
wana haki gani kwa Serikali yao waliyoiweka madarakani ambapo baada ya muda
imekuwa ikiwageuka na kuwaona hawana thamani.
Itambulike kwa ujumla wake kwamba katika zoezi la kuweka mipaka maeneo ya mapori hakukuwa na ushirikishwaji kwa
wananchi katika mambo haya ikiwemo matumizi bora ya ardhi haukufanyika hivyo
yote yaliyofanyika kuhusu utesaji,uporaji na mengine ilikuwa ni hulka kwa
wateule wa Rais ambao walilewa madaraka na kuamua kufanya watakavyo jambo
lililosababisha familia za wananchi katika maeneo mbalimbali nchini kuishi
maisha magumu ikiwamo kutokuwa na makazi,huduma za kijamii nk.
Nashauri viongozi wakuu wa Kitaifa waweke
utaratibu mzuri wa kufuatilia maagizo waliyotoa ili kuona utekelezaji maana
pindi wanapoondoka katika maeneo hayo viongozi wa chini yao hugeuka miungu watu
na kusahau maelekezo waliyopewa.
MWISHO.